Recent-Post

Maiti ya mtoto yafukuliwa Handeni, yatupwa mtaani

Waombolezaji wakiwa kwenye mazishi ya mara ya pili ya mtoto Sharifa Abasi ambaye mwili wake ulifukuliwa na watu wasiojulikana na kukutwa umetupwa mtaani. Mwili huo umezikwa tena leo katika kata ya Msasa wilayani Handeni mkoani Tanga. Picha na Rajabu Athumani.

 Siku moja baada ya mwili wa mtoto Sharifa Abasi kuzikwa, kaburi lake limefukuliwa na watu wasiojulikana huku mwili wake ukikutwa umetupwa mtaani ukiwa bado ndani ya sanda.

 Mwili huo wa mtoto ambaye aliyefariki akiwa na mwezi mmoja na wiki mbili ulizikwa jana Jumamosi Januari 8, 2022 umekutwa katika mtaa wa Msasa Shule wilayani Handeni mkoani Tanga.

Akisimulia mkasa huo baba mkubwa wa marehemu, Athumani Ligotwe wakati wa mazishi ya pili ya mtoto huyo yaliofanyika leo Jumapili asubuhi amesema ameshangazwa na tukio hilo kwani yeye ndio aliweka mwili wa marehemu kaburini jana na leo wamekutwa kaburi limefukuliwa na mwili haupo.

Amesema alifika kwenye kaburi na kubaini mwili haupo na kurudi sehemu ambayo umeonekana na kuthibitisha kuwa ulikuwa wa mtoto wa mdogo wake ambaye alizikwa jana.

Hili ni tukio la kinyama sana lililotokea kwenye familia yetu, wamefukua kaburi ya mtoto wetu na kwenda kutupa mwili mita 300 kutoka hapa kwenye nyumba ya mtu, tunaomba Jeshi la Polisi kuwatafuta hawa watu", amesema Athumani

Mkazi wa Msasa, Deo Akyoo ambaye mwili wa mtoto umekutwa kwenye uzio wa nyumbani kwake amesema usiku alisikia watu wakipita na baada ya kuamka asubuhi aliangalia na kukuta mwili wa mtoto huyo upo kwenye sanda akatoa taarifa katika uongozi wa mtaa.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Safia Jongo amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema kuwa Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na watakaobainika kufanya kitendo hicho watachukuliwa hatua za kisheria.

Sisi tunakemea tabia hii, tukio hili linaonekana kuna kitu baina ya aliyetupiwa mwili nyumbani kwake na waliofanya kitendo hicho, ila hakuna masuala ya kishirikina kwenye tukio hilo ila ni visasi tu", aamesema Kamanda Jongo.

Post a Comment

0 Comments