Kongamano hilo lililoanza tarehe 25 Machi na kufunguliwa kwa hotuba ya Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango liliwakutanisha pamoja waandishi wa habari na watangazaji wa Idhaa zinazotumia lugha ya Kiswahili duniani ili kubadilishana uzoefu katika shughuli zao za kihabari na kuleta tija zaidi katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha jamii.
Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango (mwenye miwani) akizindua toleo la tatu Kamusi ya Kiswahili katika Kongamano la Dunia la Kiswahili |
Washiriki wa Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA wametoka nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Marekani, Rwanda, Ufaransa, Uganda, Ujerumani na wenyeji Tanzania.
Wawakilishi wa redio za ndani ya Tanzania, za nje ya nchi, televisheni za kawaida na za mtandaoni, televisheni za nje ya nchi, wahadhiri wa vyuo vikuu vya ndani, wachapishaji, watu mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi 16 pamoja na wanafunzi kutoka vyuo vikuu wameshiriki katika kongamano la mwaka huu ambalo limefanyika kwa kaulimbiu "Tasnia ya Habari kwa Maendeleo Duniani.
Wazo la kuandaa Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lilianzishwa Novemba 29, 2006 na Kongamano la kwanza lilifanyika Novemba Desemba, 2007 lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu la kukieneza Kiswahili duniani kwa kukitumia na kutangaza katika vituo vyao vya habari.
0 Comments