Jiji La Dodoma Laibuka Mshindi Wa Jumla Katika Mashindano UMISSETA Dodoma

 USHIRIKIANO baina ya walimu wa michezo, wakuu wa shule na maafisa elimu umeiwezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ngazi ya Mkoa wa Dodoma ikizoa vikombe vitano vya mshindi wa kwanza katika michezo mbalimbali.


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokua akiongelea siri ya mafanikio ya timu yake katika kilele cha michezo ya UMISSETA ngazi ya Mkoa iliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Dodoma.

Mwalimu Rweyemamu alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tulijipanga vizuri. Mara tu baada ya kumaliza mashindano ya mwaka jana. Tulianza mikakati mapema kuanzia ngazi ya shule, tarafa na wilaya”.

Mkuu huyo wa Idara ya Elimu Sekondari alisema kuwa ushirikiano mkubwa baina ya walimu wa michezo, wakuu wa shule na maafisa ndiyo siri kubwa ya mafanikio kwa timu ya UMISSETA ya Jiji la Dodoma kufanya vizuri. “Wakati wa kufanya uchaguzi wa wanamichezo tulikuwa na umakini mkubwa. Tuliwachagua kwa uwezo wao na siyo kwa upendeleo. Tuliwatumia waamuzi wa nje wenye sifa kuchezesha na kufanya uchaguzi makini wa wanamichezo kwa lengo la kujenga timu imara na itakayotoa ushindani na kulinda hadhi ya Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi” alisema Mwalimu Rweyemamu.

Kwa upande wa mgeni rasmi ambae ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Aloyce Mwogofi alisema kuwa Mkoa wa Dodoma una imani kubwa na timu hiyo ya mkoa. “Sisi viongozi wa mkoa hatuna maneno mengi ya kusema, mengi mmeshaambiwa na viongozi wenu. Zingatieni taratibu za michezo hii, kwa jinsi nilivyowaona hapa nidhamu imetamalaki. Mkoa tunawatakia ushindi mkubwa, mlete jina la Dodoma kivingine” alisema Mwogofi.

Halmahauri ya Jiji la Dodoma ilikuwa mshindi wa kwanza na mshindi wa jumla ikiweka kibindoni makombe matano katika michezo wa mpira wa kikapu (wanawake), mpira wa mikono (wanawake), mpira wa mikono (wanaume), ‘basketball’ (wanaume na wanawake), na mpira wa miguu (wanawake).


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments