DAR ES SALAAM; Mbio za TASWA Mwambao Marathon zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), ambazo awali zilikuwa zifanyike mwishoni mwa mwezi uliopita sasa zitafanyika Desemba 22, 2024 jijini Tanga.
Kaimu Katibu Mkuu wa TASWA, Imani Makongoro, amesema kabla ya mbio hizo pia kutafanyika Mkutano Mkuu wa TASWA asubuhi ya Desemba 21, 2024 jijini Tanga na baadaye mchana siku hiyo kutafanyika kongamano la kitaaluma kwa wanahabari wa michezo kujadili masuala mbalimbali ikiwemo nafasi ya wanahabari kuelekea fainali za AFCON mwaka 2027.
“TASWA Mwambao Marathon 2024 ni mbio maalumu kuhamasisha wanamichezo kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kutunza mazingira na kumtua mama kuni kichwani, hivyo kusukuma mbele Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia.
“Kutokana na mazingira hayo TASWA inakaribisha mashirika ya ndani na nje, taasisi, kampuni, watu binafsi, wadau wa mazingira na nishati safi ya kupikia, kushirikiana nasi kufanikisha mbio hizo ambazo ni Kilometa 21, KM 10 na mbio za kujifurahisha (Fun Run) za KM 5. Wanaotaka kushiriki mbio hizo wanatakiwa kujisajili kwa namba ya malipo ya Tigopesa 0777333110 jina TASWA Marathon na ada ni Sh 30,000.
Isome pia: TASWA Mwambao Marathon kufanyika Tanga
“Pia kwa wanachama wa TASWA wanaotaka kushiriki Mkutano Mkuu wanatakiwa walipie ada ya uanachama ya mwaka mmoja ambayo ni Sh 30,000 kupitia benki ya CRDB, jina la akaunti Tanzania Sports Writers Association (TASWA), nambari ya akaunti ni 0133641150700, mwisho wa kuthibitisha kushriki na kulipa ada ni Novemba 25, 2024,” amesema Makongoro.
0 Comments