Wananchi wa Kata ya Kindai wameendelea kumiminika kwa pongezi na sifa tele kwa Diwani wao, Mheshimiwa Omary Salum Kinyeto, wakimtaja kuwa ni kiongozi shupavu, mwenye maono na anayejali maslahi ya wananchi wake katika kila hatua ya uongozi wake tangu mwaka 2020.
Katika mahojiano na wakazi mbalimbali wa mitaa ya Kilambida, Mahembe, Kindai, Kibaoni, Dodoma Road, Bohari na Singida Mnangi, wananchi wamesema hawana shaka kuwa maendeleo yanayoonekana ni matokeo ya jitihada binafsi za Mheshimiwa Diwani Kinyeto kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali.
“Tumeshuhudia miradi mikubwa ikitekelezwa kama ujenzi wa madarasa, barabara za lami, vyoo, ofisi za walimu na upatikanaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana. Haya yote yametokea kwa sababu tuna diwani anayesimama na wananchi wake,” alisema Bi. Sara Seti mkazi wa Kilambida.
Katika sekta ya elimu pekee, chini ya uongozi wake, Kindai Sekondari imepata madarasa mapya, vyoo, maabara na nyumba za walimu zimeanza kujengwa. Hali ya uandikishaji wanafunzi imeongezeka huku uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia ukiwa wa kuridhisha.
Aidha, kwa upande wa miundombinu, barabara ya lami ya Kibaoni-Mahembe imekamilika sambamba na ujenzi wa kivuko cha chini (underpass) katika mtaa wa Kibaoni, mradi uliogharimu zaidi ya Tsh bilioni 2 – jambo ambalo wananchi wanasema halijawahi kutokea katika historia ya kata hiyo.
“Mheshimiwa Kinyeto si tu kwamba anaongea, bali anatenda. Amehakikisha tunapata huduma za msingi kama maji, elimu bora, usafi wa mazingira na hata ulinzi wa kutosha kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi,” alieleza Bw. Emmanuei Robart wa Mahembe.
Wananchi pia wamesema kuwa kwa mara ya kwanza, wameona magari ya kuzoa taka yakifika mtaani kila Ijumaa, jambo lililosaidia kuimarisha usafi wa mazingira, huku juhudi za upandaji wa miti zaidi ya 5,700 zikifanikishwa chini ya uongozi wake.
“Mheshimiwa Kinyeto ameonyesha kuwa uongozi si maneno, ni vitendo. Tumeona miradi mingi imetekelezwa, na hata changamoto zilizopo kama uhaba wa nyumba za walimu na maji, anazisimamia kwa karibu ili zipatiwe suluhisho,” alisema Bi. Janeth kutoka Kindai Bohari.
Wananchi hao wamempongeza pia kwa kuimarisha hali ya usalama, kuendeleza utawala bora na kushirikiana na mashirika ya maendeleo kama Faraja Centre, Helvetas na Outreach kuhakikisha jamii ya Kindai inakuwa imara kijamii na kiuchumi.
Kwa pamoja, wakazi wa Kata ya Kindai wametoa rai kwa uongozi wa juu wa Serikali na Chama kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Omary Kinyeto ili aweze kuendeleza jitihada zake za kuiletea Kindai maendeleo ya kweli na endelevu.
0 Comments