MBIO ZA URAIS 2025: CUF YASEMA:HAKI KWANZA

 


Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-Dodoma

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, amechukua rasmi fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania kiti cha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akiwa na mgombea mwenza wake, Husna Mohammed Abdalla.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, Gombo alisisitiza kuwa kipaumbele kikuu cha CUF ni haki kwa wote, akisema taifa haliwezi kuendelea endapo baadhi ya wananchi wananyimwa huduma za msingi.

“Katika Tanzania ya leo, wapo wanaopata huduma bora za afya na wengine wakikosa, wapo wanaopata elimu ya kiwango cha juu na wengine wakisahaulika kabisa,huu ni mgawanyiko usiokubalika katika taifa lenye rasilimali za kutosha,” alisema Gombo.

Mgombea huyo alibainisha kuwa serikali ya CUF, iwapo itapata ridhaa ya wananchi, itahakikisha haki katika elimu na afya inatekelezwa kwa vitendo, ili rasilimali za taifa zitumike kwa manufaa ya Watanzania wote bila ubaguzi.

“Tumechoka kuona keki ya taifa ikigawanywa kwa wachache, wakati mamilioni ya wananchi wakiachwa kando,Serikali yetu itapigania usawa wa huduma, usawa wa fursa, na usawa wa heshima kwa kila Mtanzania,” ameongeza.

Kwa sasa, CUF iko katika hatua ya kuimarisha mtandao wake wa wadhamini na kuandaa sera za kina, ambazo mgombea huyo amesema zitakuwa dira ya kuondoa pengo lililopo kati ya wenye nacho na wasio nacho, na kujenga taifa la haki na mshikamano wa kweli.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments