Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema kuwa wafanyabiashara wa maduka pamoja na wananchi wa Mkoa wa Singida wanaendelea kunufaika na mazingira bora ya uongozi na maendeleo chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa mafunzo maalum yaliyotolewa kwa madiwani wa Mkoa wa Singida kuhusu utawala bora, ushirikiano kati ya viongozi wa wananchi na watumishi wa Serikali pamoja na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dendego alisema Mkoa wa Singida umeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali kutokana na mshikamano wa viongozi pamoja na maono ya viongozi wenye nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
Alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, ameendelea kuwa mfano wa uongozi wa karibu na wananchi kwa kusimamia maendeleo, kuhimiza uwajibikaji na kuunganisha viongozi katika kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo.
“Leo hii wafanyabiashara wa maduka pamoja na wananchi wa Singida wanafanya shughuli zao kwa matumaini makubwa kutokana na mazingira mazuri ya uongozi yaliyojengwa chini ya Mama Mlata. Ni kiongozi mwenye maono mapana na anayejali maendeleo ya watu wake,” alisema Dendego.
Aidha, Dendego aliwataka madiwani kuhakikisha wanashirikiana vizuri na watumishi wa Serikali katika maeneo yao ili kuongeza kasi ya maendeleo na kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.
Alieleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji wa Serikali ni msingi muhimu katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na kufanikisha miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kwa upande wake, baadhi ya madiwani waliohudhuria mafunzo hayo walieleza kuwa semina hiyo imewajengea uwezo mkubwa wa kiuongozi na kuwapa mwanga kuhusu namna bora ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, mshikamano na uwajibikaji.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Mkoa wa Singida umeendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu pamoja na biashara, hali inayotajwa kuchangiwa na ushirikiano wa viongozi wa Serikali na chama katika kusimamia maendeleo ya wananchi.
Wananchi wa Singida wameendelea kueleza matumaini yao kwa viongozi wanaoweka mbele maslahi ya jamii, huku jina la Martha Mlata likitajwa mara kwa mara kama mmoja wa viongozi wenye mchango mkubwa katika kuimarisha mshikamano na maendeleo ndani ya Mkoa wa Singida.
Na Abdul Ramadhani Singida Tanzania





0 Comments