Chief Thomas Mgonto Aendelea na Ziara ya "Skonga Mtaa kwa Mtaa", Atoa Elimu na Kukutana na Wananchi Kata ya Issuna

                                  

Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Chief Thomas Mgonto, ameendelea na utekelezaji wa ziara yake ya "Skonga Mtaa kwa Mtaa", ambapo safari hii alifika katika Kata ya Issuna kwa lengo la kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.

Katika ziara hiyo, Chief Mgonto alitembelea taasisi za elimu ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi na kuwapa hamasa kuhusu umuhimu wa elimu, nidhamu, kujituma katika masomo na kujenga maadili mema yatakayowasaidia kufikia malengo yao ya baadaye.

Akizungumza na wanafunzi, aliwahimiza kutumia ipasavyo muda wao wa masomo, kuwaheshimu walimu na wazazi, pamoja na kuamini kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

Mbali na shughuli za elimu, Mbunge huyo aliendelea kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi kupitia programu ya "Skonga Mtaa kwa Mtaa", inayolenga kusikiliza maoni, changamoto na mapendekezo ya wananchi ili kuchangia katika kupanga vipaumbele vya maendeleo ya Jimbo la Ikungi Mashariki.

Wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walipata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na maendeleo, huku wakieleza matarajio yao ya kuendelea kushirikiana na viongozi katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.

Ziara ya "Sikonga Mtaa kwa Mtaa" inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ikungi Mashariki ikiwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi kupitia mawasiliano ya karibu na ushiriki wa moja kwa moja katika shughuli za maendeleo.

Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments