LWANJI AZINDUA MUBASHA BONANZA CUP MANYONI SINGIDA

Hamasa ya michezo imezidi kushika kasi katika Wilaya ya Manyoni baada ya Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Singida, Eliphas Lwanji, kuzindua rasmi mashindano ya Mubasha Bonanza Cup yaliyofanyika katika Kata ya Kintinku, yakilenga kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha mshikamano wa jamii kupitia michezo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lwanji alisema michezo ni chombo muhimu cha kujenga taifa kwa kuwa huibua vipaji, hujenga afya, huimarisha nidhamu na huwapa vijana fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aliwataka vijana kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia nidhamu, ushindani wa haki na kuheshimu sheria za mchezo, akisisitiza kuwa ushindi wa kweli unaambatana na maadili mema ndani na nje ya uwanja.

"Vijana ndiyo nguvu ya Taifa. Tuilinde amani yetu, tufanye kazi kwa bidii na tutumie michezo kama daraja la kuonesha vipaji vyetu na kujijengea maisha bora. Amani ndiyo msingi unaowezesha michezo na maendeleo kustawi," alisema Lwanjo.

Aidha, alieleza kuwa Mubasha Bonanza Cup ni jukwaa muhimu la kuibua vipaji vipya vitakavyoweza kuonekana na kusajiliwa na klabu mbalimbali za ngazi ya wilaya, mkoa na hata Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika hafla hiyo, Lwanji alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Dkt. Pius Chaya, kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo kama nyenzo ya kuwawezesha vijana.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Chaya alisema ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya maendeleo ya vijana wa Manyoni, akibainisha kuwa vipaji vinahitaji kupewa mazingira bora ili viweze kukua na kuwafikisha vijana katika ngazi za juu za ushindani.

"Tunaamini michezo ni sehemu ya maendeleo ya jamii. Tutaendelea kuunga mkono mashindano kama haya kwa sababu yanajenga umoja, yanaibua vipaji na yanatoa fursa kwa vijana wetu kutimiza ndoto zao," alisema Dkt. Chaya.

Kwa upande wao, waandaaji wa Mubasha Bonanza Cup wamesema mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuendeleza michezo katika ngazi ya jamii, kuimarisha mshikamano wa vijana na kutoa jukwaa la kuonesha vipaji vinavyoweza kufungua milango ya ajira kupitia sekta ya michezo.

Uzinduzi huo uliambatana na shamrashamra mbalimbali za michezo, huku mamia ya wananchi wa Kata ya Kintinku na maeneo jirani wakijitokeza kushuhudia mwanzo wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Timu zinazoshiriki zinatarajiwa kuonesha kiwango cha juu cha soka katika harakati za kutwaa ubingwa wa Mubasha Bonanza Cup.

Mashindano hayo yanaendelea kuonesha namna ambavyo michezo imekuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii, kuhamasisha amani, kukuza vipaji na kuandaa kizazi cha vijana wenye nidhamu, uzalendo na uwezo wa kushindana katika viwango vya juu vya soka nchini. Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments