Watu 12 wamefariki dunia, wakiwemo askari Polisi watano na mahabusu saba, katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Mlima Sekenke, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Amon Kakwale, amesema ajali hiyo imetokea Septemba 21, 2026, majira ya saa 2:00 asubuhi, baada ya gari la tanki la mafuta lenye namba za usajili RAF 245X, likiwa na tela lenye namba RL 4255, kugongana na gari ndogo ya Jeshi la Polisi yenye namba PT 1982, aina ya Toyota Land Cruiser.
Kwa mujibu wa Kamanda Kakwale, gari hilo la tanki lilikuwa likitokea Singida kuelekea Tabora, wakati gari la Polisi lilikuwa likiwasafirisha mahabusu na askari kuelekea Mahakama ya Kiomboi.
Amesema gari la Polisi lilikuwa limebeba mahabusu wanane na askari Polisi watano, akiwemo afisa mmoja aliyekuwa Mkuu wa Kituo.
Katika ajali hiyo, watu 12 walipoteza maisha, huku watu wawili wakijeruhiwa. Miongoni mwa majeruhi ni mahabusu mmoja pamoja na dereva wa lori la tanki la mafuta.
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa tanki kushindwa kulimudu gari hilo na kuelekea upande wa kulia, hivyo kuligonga gari hilo uso kwa uso,” amesema Kamanda Kakwale.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Mandewa, huku majeruhi wakiendelea kupata matibabu.
Kamanda Kakwale amesema Jeshi la Polisi limeanza taratibu za kuandaa miili ya askari waliofariki kwa ajili ya kusafirishwa kwenda maeneo yao ya asili, ambapo taratibu za mazishi zitafanyika kwa mujibu wa taratibu na mila husika.
Aidha, Kamanda Kakwale amewataka madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, pamoja na kufuata alama na maelekezo ya barabarani, hususan katika maeneo yenye miteremko na kona kama Mlima Sekenke.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini kwa kina mazingira na sababu zilizosababisha ajali hiyo.
Na Saulo Stivin Singida Tanzania

0 Comments