Akizungumza mbele ya mamia ya wanachama na wapenzi wa chama hicho, Dkt. Mwigulu alisema wananchi wa Singida wameona na kuguswa na maendeleo makubwa yaliyotekelezwa chini ya uongozi wa CCM, hivyo hawana sababu ya kugeuka.
“Tunamuhakikishia Katibu Mkuu wetu, Dkt. Nchimbi, kuwa Singida ni ngome ya kweli ya CCM. Tumejipanga kuhakikisha wagombea wetu wote wanapata kura za kishindo. Wananchi wameona kazi, wameona matokeo, na sasa wako tayari kulinda mafanikio haya kwa kura,” alisema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan umeweka historia mpya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini, ikiwemo miradi ya maji, barabara, afya na elimu mkoani Singida, jambo lililoongeza imani kubwa kwa wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi.
“Dkt. Samia ametuonesha dira ya kweli ya maendeleo. Hivyo sisi kama wana-CCM na wananchi wa Singida tumeamua — tutampigia kura kila mgombea wa CCM kwa kishindo. Huo ndio uthibitisho wa shukrani yetu kwa kazi kubwa iliyofanyika,” aliongeza.
Kwa upande wake, viongozi wa chama na jumuiya mbalimbali waliomshuhudia wakionyesha imani kubwa kwa kauli hiyo, walisema Singida itaendelea kuwa mfano wa umoja na uaminifu ndani ya CCM, huku wakiahidi kuendelea kusimamia kampeni zenye maadili na zenye kuhamasisha maendeleo.

0 Comments