DK. MWIGULU AANZA KWA KASI: AZUIA WAJAWAZITO KUSUBIRISHWA MAPOKEZI, ATOA MAAGIZO MAZITO HOSPITALI NCHINI

 



Na Dotto Kwilasa,DODOMA

Katika mwanzo wenye kasi na ujumbe thabiti kuhusu maboresho ya huduma za afya nchini, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ameanza rasmi majukumu yake kwa kufanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na kupiga marufuku utaratibu uliokuwa ukiwachelewesha wajawazito kupata huduma pindi wanapofika wakiwa na uchungu wa kujifungua.

Ziara hiyo imefanyika mapema leo November 15,2025 ikiwa ni siku moja tu baada ya kuapishwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo alichagua kuanza na sekta inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja ambayo ni afya.

Katika ziara hiyo, Dk. Nchemba amezungumza na watumishi, wagonjwa na jamaa waliokuwepo hospitalini, akitaka kusikia moja kwa moja namna wanavyohudumiwa.

Amepitia wodini, akahoji changamoto za matibabu, upatikanaji wa dawa na mwenendo wa huduma za dharura, hasa kwa akinamama wajawazito.

Baada ya kukamilisha ukaguzi, alitoa maagizo mazito kwa hospitali zote nchini ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mama mjamzito kusubirishwa mapokezi wakati ana uchungu wa kujifungua.

"Wajawazito wapate huduma kwanza,kama ni kuandikishwa, afatwe wodini,” amesisitiza.

Aidha, ameonesha kutoridhishwa na taarifa kwamba baadhi ya wajawazito wanashindwa kuhudumiwa kwa wakati kutokana na kukosa ndoo ama beseni, akisema haitarajiwi mama mjamzito kuzuiliwa na suala la vifaa vidogo ambavyo hospitali inapaswa kuwa navyo kama tahadhari.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliagiza Wizara ya Afya na MSD kuhakikisha hospitali zinanunua dawa kulingana na mahitaji halisi ya maeneo husika badala ya kuweka kipaumbele kwenye vipimo pekee kisha kuacha wagonjwa wakitangatanga maduka binafsi kutafuta dawa.

“Haiwezekani hospitali ya umma ikose dawa lakini maduka ya jirani yapate,huu mchezo wa kuagiza panado kidogo ili wengine wanunue nje Sitarajii kuuona tena.”amesisitiza

Hata hivyo, pamoja na mapungufu aliyoyaona, Dk. Nchemba ameridhishwa na maeneo kadhaa ya utoaji huduma na kuagiza changamoto zilizopo zifanyiwe kazi kwa haraka.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ibenzi Ernest, amemshukuru Waziri Mkuu kwa uamuzi wa kufanya ziara hiyo ya kushtukiza akisema imeongeza hamasa kwa watumishi.

“Tunafurahi kututembelea,ahadi zake na maagizo yake yatatuongezea uwajibikaji na ufanisi.”ameeleza

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments