MSIGWA ATAKA VIJANA KUEPUKA UCHOCHEZI WA WATU WALIO NJE YA NCHI

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametoa wito kwa wananchi, hususani vijana, kujiepusha na vitendo vya uchochezi vinavyopandikizwa na watu wanaoishi nje ya nchi na ambao hawaguswi na madhara ya matendo wanayohamasisha yafanyike ndani ya Tanzania kwa kisingizio cha kudai haki.

Ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuelezea athari za vurugu na uvunjifu wa amani vilivyotokea Siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuatia. Amesema vurugu hizo zimewaumiza Watanzania wenyewe, huku wale wanaochochea wakibaki salama katika mataifa ya mbali “wakila na kuishi bila wasiwasi.”

“Nawasihi Watanzania kujiepusha kushabikia au kusambaza taarifa zinazochochea hasira na kuvunja umoja wetu wa kitaifa. Tukiendekeza uchochezi unaofanywa na watu walioko nje ya nchi na wasioguswa na maisha yetu, watakaoumia ni sisi,” amesema Msigwa.

Amehimiza wananchi kuendelea kuwa watulivu na kukataa kutumika katika matendo yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi, akibainisha kuwa Serikali ipo tayari kusikiliza changamoto, madai, ushauri na maswali kutoka kwa makundi mbalimbali kwa mujibu wa taratibu na sheria.

“Hakuna sababu ya kuharibu nchi. Kama kuna changamoto, zifikishwe serikalini ili zifanyiwe kazi ndani ya mfumo uliowekwa,” amesisitiza.

Aidha, Msigwa ameonya kuwa athari za kuvuruga utulivu wa nchi zitawaangukia Watanzania wenyewe na si wale wanaochochea kutoka mbali. Amesema baadhi ya watu hutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kupandikiza hasira na mfarakano ili waamshiwe vitendo vya uharibifu.

“Lengo la watu wanaotengeneza chokochoko mtandaoni ni kuwachochea vijana wafanye uharibifu, ilhali wao wako salama. Ni muhimu kutokubali kutumiwa,” ameongeza.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments