Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameanza safari mpya ya kusimamia uwajibikaji katika miradi ya serikali baada ya kutoa agizo la kukamatwa kwa Mkandarasi anayehusika na ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari cha Muhalala, wilayani Manyoni mkoani Singida.
Mradi huo ambao ulilenga kuboresha usalama wa barabarani na kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa magari ya mizigo na abiria, umedumu kwa zaidi ya miaka nane bila kukamilika, hali iliyowakasirisha wananchi na kuilazimu serikali kuchukua hatua kali.
Katika mkutano wake na wananchi, Mwigulu alitoa maelekezo kwa Kamishna wa Uhamiaji kuhakikisha mkandarasi huyo anakamatwa na kushikiliwa, huku hati yake ya kusafiria ikitaifishwa mpaka mradi huo ukamilike.
Waziri Mkuu amesema serikali haiwezi kuendelea kuvumilia uzembe unaochelewesha maendeleo na kusababisha hasara kwa taifa.
Mwigulu Nchemba — Waziri Mkuu:
“Hatutaendelea kuvumilia uzembe unaochelewesha maendeleo. Hati yake ya kusafiria isishikiliwe mpaka amalize mradi huu.”
Waziri Mkuu hakusita kwenda mbali zaidi. Ametaka washirika wote wa mkandarasi husika kufika wizarani na kutoa maelezo ya kina juu ya hatma ya mradi huo.
Amesema ikiwa hawatatoa taarifa sahihi na za kutosha, serikali italazimika kuchukua hatua kali zaidi ikiwemo kuvunja mkataba na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.
Mwigulu Nchemba:
“Tunataka majibu ndani ya muda mfupi. Washirika wake watueleze kama wanaendelea na mradi au wameutelekeza.”
Hatua hii imeonyesha dhamira ya serikali kuzuia mianya ya uvunjifu wa maadili katika sekta ya ujenzi na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi.
Katika hotuba yake, Mhe. Mwigulu pia aliwataka vijana kutumia nguvu zao katika kulinda maslahi ya taifa, kuzingatia nidhamu, na kuhakikisha miradi inalindwa dhidi ya wizi, ufujaji au hujuma.
Mwigulu:
“Vijana mlio hapa, nchi ni yenu. Aineni na simameni kulinda maslahi ya taifa.”
Amesema taifa haliwezi kusonga mbele ikiwa vijana hawataungana kupigania uadilifu na uwajibikaji.
Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Abdala Ulega, amesisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wasiokamilisha kazi kwa wakati.
Amesema ucheleweshaji wa mradi kwa miaka nane ni ishara ya uzembe uliopitiliza, na serikali haiwezi kuendelea kufumbia macho vitendo vya aina hiyo.
Wananchi wa Manyoni wamesema hatua ya Waziri Mkuu imewasisimua na kuleta matumaini mapya kuwa mradi huo muhimu sasa utakamilika.
Ismail Mrisho na Juma Alute wamesema kuwa kwa mara ya kwanza serikali imeonyesha msimamo thabiti katika kuwawajibisha waliokwamisha maendeleo ya eneo hilo.
Wamesema kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza msongamano wa magari, kuongeza mapato ya serikali, na kuboresha usalama wa barabarani.

Na Abdul B. Ramadhani Singida Manyoni.







0 Comments