Mwanasiasa kijana na mkongwe katika harakati za maendeleo katika mkoa wa Singida akiwa katika ya Jimbo la Itigi, Martini Lisu, amezungumza kwa hisia kali kuhusu uamuzi wa Yohana Msita kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliowakutanisha viongozi wa kata wananchi , vijana na wazee wa kimila, Lisu alisema kuwa hatua ya Msita haikuwa ya bahati mbaya, bali ni matokeo ya maombi, imani na utayari wa kuchukua jukumu la kuwatumikia wananchi.
“Uongozi si ushawishi wa mitandao, si upepo wa siasa za muda mfupi. Uongozi hupangwa na Mungu. Msita kuchukua fomu si ajali ya kisiasa—ni wito aliopangiwa,” alisema Lisu kwa uchungu na msisitizo.
Lisu alifafanua kuwa Msita ni miongoni mwa viongozi wachache wanaoheshimika kwa uwazi, busara na nidhamu katika utumishi wa umma, na kwamba amekuwa akitekeleza majukumu ya kijamii kwa muda mrefu bila kutafuta sifa.
Aidha, aliwataka wananchi wa Itigi kuangalia zaidi mwenendo, fikra na moyo wa mbunge kuliko kelele na propaganda zinazoenezwa na baadhi ya makundi yenye maslahi binafsi.
Kiongozi huyo pia alisisitiza umuhimu wa umoja, akisema kuwa mgawanyiko wa kisiasa usio na tija unaweza kurudisha nyuma maendeleo yaliyokwisha kupatikana.
“Msita hakuamka tu asubuhi na kuamua kuchukua fomu. Amevumilia, ameomba, ameshauriwa, na zaidi ya yote—ameitwa. Tukimpa nafasi, Itigi itapiga hatua,” aliongeza Lisu.
Hata hivyo, Lisu aliweka wazi kuwa safari ya kisiasa si rahisi, akisisitiza kuwa kila mgombea ana changamoto zake, lakini watu wanaongozwa na Roho ya Mungu kamwe hawawezi kushindwa.
Mwisho wa hotuba yake uliamsha hisia kubwa miongoni mwa hadhira, wengi wakimpongeza kwa kusema ukweli bila kificho na kutetea maadili ya uongozi ndani ya chama na jimbo kwa ujumla.
Na Abdul Bandola Singida





0 Comments