Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mosses Mlata, ameendelea na ziara yake ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake pamoja na kuwashukuru viongozi na wanachama kwa ushiriki wao mkubwa katika ushindi wa CCM kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambapo leo ziara hiyo imefanyika Wilaya ya Iramba.
Ziara hiyo ni sehemu ya muendelezo wa kampeni ya kuimarisha mshikamano ndani ya Chama baada ya awali kufanyika katika Wilaya za Manyoni na Ikungi, huku ikikusanya mamia ya wananchi, viongozi na wanachama waliojitokeza kumpokea na kusikiliza ujumbe wake wa kisiasa na kijamii.
Akizungumza mbele ya viongozi na wananchi wa Iramba, Martha Mlata amesema kuwa CCM itaendelea kusimamia kwa nguvu zote misingi ya umoja, mshikamano na uwajibikaji ili kuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara na chenye kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Amesisitiza kuwa maadili ya jamii ni msingi muhimu wa kulinda amani, upendo na mshikamano wa Taifa, hivyo viongozi na wananchi wanapaswa kuendelea kuyasimamia kwa vitendo katika maisha ya kila siku.
Tunapaswa kuendelea kulinda maadili yetu ya Kitanzania ili kuimarisha amani na mshikamano katika jamii yetu, kwa sababu amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mlata.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Singida amewapongeza viongozi, wanachama na wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu uliopita na kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi.
Amesema ushindi mkubwa uliopatikana unatokana na imani ya wananchi kwa CCM pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Wananchi wa Iramba waliopata nafasi ya kushiriki katika mkutano huo wameeleza kufurahishwa na ziara ya Martha Mlata, wakimtaja kuwa ni kiongozi mwenye maono, anayejali wananchi na mwenye uwezo mkubwa wa kuunganisha jamii kupitia sera na misingi ya Chama Cha Mapinduzi.
Ziara hiyo imeendelea kuacha alama kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Singida huku ikiongeza hamasa mpya ya kuendelea kuijenga CCM pamoja na kuimarisha ushirikiano katiya viongozi na wananchi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
Na abdul Ramadhani Singida Tanzania
0 Comments