Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya kaya zenye uhitaji nchini kwa kuwawezesha wananchi, hususan wanawake, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.
Mafanikio hayo yamebainishwa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika jijini Dodoma, ambapo TASAF ilitoa fursa kwa baadhi ya wanufaika wa mpango huo kuonesha bidhaa na huduma zao katika banda la maonesho.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa taasisi hiyo, Bw. Uswege Edward, alisema ushiriki wa wanufaika katika maonesho hayo ni sehemu ya kuonesha matokeo chanya ya utekelezaji wa TASAF Awamu ya Pili.
Alieleza kuwa wanufaika kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wameweza kupata msaada mbalimbali ikiwemo mitaji, vifaa vya uzalishaji na fursa za maendeleo zilizowawezesha kuanzisha au kukuza biashara zao.
“Tunajivunia mafanikio ya walengwa wetu. Wakati wa usajili, baadhi yao walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa za maisha, ikiwa ni pamoja na kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku. Leo hii wengi wao wanaendesha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowapa kipato na kuwasaidia kujitegemea,” alisema Bw. Uswege.
Aliongeza kuwa TASAF imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwawezesha wananchi kujiondoa katika mzunguko wa umaskini kwa kuwapa nyenzo na fursa za kuboresha maisha yao na ya familia zao.
Kwa mujibu wa TASAF, mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha hali ya maisha ya kaya nyingi nchini, huku ukitoa nafasi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Devota Karia, alisema amepata manufaa makubwa kupitia TASAF na kwamba kushiriki katika maonesho hayo kumemsaidia kutangaza biashara yake na kupata wateja wapya.
“Tunashukuru kupata nafasi hii ya kuonesha bidhaa zetu. Maonesho haya yametupa fursa ya kujifunza, kutangaza biashara na kukutana na wateja wapya,” alisema Devota.
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa programu za maendeleo ya jamii ambazo zimeleta matumaini mapya kwa maelfu ya wananchi wenye uhitaji.
TASAF imeendelea kuwa moja ya programu muhimu za maendeleo nchini, ikilenga kuimarisha ustawi wa kaya maskini kupitia uwezeshaji wa kiuchumi, elimu, afya na huduma nyingine za msingi. Kupitia juhudi hizo, wananchi wengi wameanza kujenga maisha yenye matumaini na uwezo mkubwa wa kujitegemea.

0 Comments