WAZIRI KAPINGA AMKABIDHI MJASIRIAMALI MWENYE ULEMAVU MASHINE YA KUSAGIA VIUNGO, ATOA MAELEKEZO KWA TAASISI ZA SERIKALI KUMWEZESHA KUKUA KIBIASHARA

 

 Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amemkabidhi mfanyabiashara mwenye ulemavu, Bi. Esther Mashaka Msengi, mashine ya kusagia viungo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwawezesha wajasiriamali kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuboresha kipato.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo Waziri Kapinga alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali, ikiwemo watu wenye ulemavu, ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Alieleza kuwa aliamua kumsaidia Bi. Esther baada ya kubaini changamoto aliyokuwa akiikabili ya kusafirisha viungo kwenda kusagwa katika maeneo mengine, hali iliyokuwa ikiongeza gharama za uzalishaji na kutumia muda mwingi kabla ya bidhaa kufika sokoni.

"Upatikanaji wa mashine hii utarahisisha mchakato wa uzalishaji, kuongeza ufanisi wa biashara na kumwezesha mjasiriamali huyu kuongeza thamani ya bidhaa zake," alisema Waziri Kapinga.

Katika kuhakikisha biashara ya Bi. Esther inakuwa endelevu, Waziri Kapinga alizielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu.

Aliitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kukamilisha usajili wa nembo ya bidhaa zake, huku Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likielekezwa kumsaidia kupata ithibati ya ubora wa bidhaa zake ili ziweze kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, alilitaka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuendelea kumpatia mafunzo na huduma za maendeleo ya biashara zitakazomwezesha kuongeza uwezo wa uzalishaji na ushindani.

Waziri Kapinga pia alilishukuru Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine hiyo, akisema hatua hiyo inaendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wajasiriamali kuongeza tija, ajira na mchango wao katika uchumi wa nchi.

Akizungumza baada ya kupokea mashine hiyo, Bi. Esther Mashaka Msengi alisema msaada huo utakuwa chachu ya maendeleo ya biashara yake kwa kuwa utapunguza gharama za uzalishaji, kuongeza kasi ya usindikaji wa viungo na kumwezesha kupanua wigo wa masoko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa TEMDO, Mhandisi Elisante Mjema, alisema mashine iliyotolewa ina uwezo wa kusaga hadi kilo 10 za viungo kwa saa moja, jambo litakaloongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

Aliongeza kuwa, endapo kutakuwa na upatikanaji wa malighafi za kutosha pamoja na soko la uhakika, uzalishaji huo unaweza kufikia mauzo ya takribani shilingi milioni 1.5 kwa siku, hatua inayoweza kuongeza mapato ya mjasiriamali na kuchochea ukuaji wa biashara yake.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwawezesha wajasiriamali, hususan makundi yenye mahitaji maalum, kupitia teknolojia, mafunzo na ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kuimarisha maendeleo ya uchumi jumuishi.

        

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments