DC MPOGOLO AAGIZA TCRA KUANDIKIWA BARUA KUZAGAA KWA NYAYA BARABARANI

 HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam limeelekezwa kuandika barua kwenda kwa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuchukua hatua kuhakikisha kampuni za mawasiliano zinaondoa nyaya zilizotelekezwa mitaani na zilizowekwa bila mpangilio.


Maelekezo hayo yametolewa leo Oktoba 10 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo baada ya kufanyika kwa usafi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambapo pia watumishi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Mkurugenzi wa Jiji hilo Elihuruma Mabelya wameshiriki kufanya usafi .

“Baadhi ya kampuni zimekuwa zikitandaza nyaya bila kuzisimamia ipasavyo. Nyaya zisizotumika huachwa ovyo barabarani, kwenye mifereji na maeneo mengine ya umma.Hivyo nakuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam uwaandikie barua rasmi TCRA ili nao wawaandikie barua kampuni zinazosambaza waya.

“Ukiangalia katika Jiji la Dar es Salaam kumekuwa na nyaya ambazo zimewekwa bila mpangilio,zimekuwa kama uchafu .Kuna maeneo nyaya ziko chini zimezagaa katika barabara na katika mitaro,”amesema Mpogolo.

Amefafanua kampuni zitakiwa kurekebisha hali hiyo na kwamba zipewe muda maalumu wa kuondoa nyaya zilizotelekezwa huku akisisitiza wale watakaokadi hatua za kisheria zitachukuliwa.

Ameongeza hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Halmashauri na TCRA na mkakati ni kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa safi, salama na lenye mazingira bora kwa wakazi na wafanyabiashara.

Akizungumzia hali ilivyo Kariakoo, alisema wingi wa nyaya zilizotandazwa katika maeneo mbalimbali unafanya baadhi ya sehemu kuonekana kama zimefunikwa na utando wa buibui. Hali hiyo inaharibu mwonekano wa eneo hilo lenye shughuli nyingi za biashara.

Pia amesema nyaya hizo zinaweza pia kuathiri shughuli za uokoaji wakati wa dharura, ikiwemo operesheni za zimamoto. Pia zinaweza kuingilia shughuli za wafanyabiashara wanaotumia makontena kuingiza na kutoa mizigo katika eneo hilo.

Amesema baadhi ya nyaya zilizotelekezwa zimetapakaa barabarani na kuingia kwenye mifereji ya maji ya mvua na mifereji ya chini ya ardhi. Hali hiyo inaweza kusababisha mifumo hiyo kuziba na kuongeza changamoto za usafi.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, hali hiyo pia inaongeza mzigo wa kazi kwa watumishi wa usafi. Wanaposhughulikia taka katika maeneo ya umma, hulazimika pia kuondoa nyaya zilizoachwa na kampuni baada ya kukamilisha kazi zao.

Amesema kampuni zinapaswa kuhakikisha nyaya zinazoondolewa au zisizotumika hazitelekezwi katika maeneo ya umma.

Wakati huo huo Mpogolo amewataka wadau kutambua jukumu la kuifanya Dar es Salaam kuwa safi si la Halmashauri pekee bali ni jukumu la mdau.





TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments