Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amezindua rasmi tovuti ya Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT) katika Kongamano na Mkutano Mkuu wa Chama hicho, jijini Dodoma.


Uzinduzi huo umefanyika mara baada ya kufungua Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini nchini Tanzania, lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho, uliofanyika Oktoba 31,2026 jijini Dodoma.

Aidha, Msigwa amewataka waandishi wa habari kupaza sauti za wananchi wanaoishi vijijini, kuwasaidia kupata taarifa sahihi na kuibua suluhisho la changamoto zinazozikabili jamii hizo.
Msigwa ameipongeza RUJAT kwa kuanzisha tovuti hiyo, akieleza kuwa itachangia upatikanaji wa habari mbalimbali, kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi na kuchochea maendeleo.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini na mwanahabari mwandamizi, Ester Bulaya, amewataka waandishi wa habari kuwa wabunifu, kufanya tafiti na uchunguzi, pamoja na kurejea misingi ya uandishi wa habari wa zamani ili kukuza ushindani wa kitaaluma.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Chama kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, amesema RUJAT imefanikiwa kuanzisha tovuti rasmi ya Chama kupitia anuani ya www.rujat.or.tz.

“Hili ni fanikio muhimu katika safari ya kukua na kuimarika kwa Chama, hususan katika zama ambazo teknolojia ya habari na mawasiliano ina nafasi kubwa katika kujenga taasisi imara na kuunganisha wadau,” amesema Kwigize.

Amesema kuanzishwa kwa tovuti hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha utambulisho wa RUJAT kwenye majukwaa ya kidijitali, kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu Chama na shughuli zake, pamoja na kuongeza mwonekano wake kwa wanachama, taasisi za serikali, wadau wa maendeleo, washirika wa kimataifa na umma kwa ujumla.

Pia, tovuti hiyo inaweka msingi wa RUJAT kuwa na jukwaa lake rasmi la kutangaza shughuli, mafanikio, fursa za ushirikiano, programu za maendeleo na habari zinazohusu waandishi wa habari za vijijini.

Kwigize amesema uwepo wa tovuti rasmi unaongeza fursa kwa Chama kujenga uaminifu wa kitaasisi, kupanua mtandao wa wadau na kuimarisha mawasiliano yanayovuka mipaka ya kijiografia.

Katika kipindi kijacho, RUJAT imelenga kuendeleza matumizi ya tovuti hiyo kwa kuhakikisha inasasishwa mara kwa mara na kuwa chanzo cha kuaminika cha taarifa kuhusu Chama, shughuli zake na mchango wa waandishi wa habari za vijijini katika maendeleo ya jamii.

Kongamano hilo la RUJAT lilibebwa na kaulimbiu isemayo: “Kuimarisha Uandishi wa Habari za Vijijini kwa Maendeleo Endelevu, Utawala Bora na Ustawi wa Jamii.”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560