SERIKALI imesema kuwa, kushamiri kwa vitendo vya ukatili nchini ni matokeo ya wananchi kutokuwa na mawazo chanya kuhusu shughuli za Maendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula ameyasema hayo wakati aliposhiriki kwenye kikao kazi cha Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa (TOA) chenye lengo la kujenga uelewa wa ugatuaji madaraka kwa wananchi, jijini Dodoma Februari 21, 2023
Dkt. Chaula ameeleza kuwa, wananchi wakibadili fikra na mitazamo ya kujiletea Maendeleo wao wenyewe kwa kubuni na kupanga, vitendo vya ukatili vitapungua na kuisha kabisa.
"Nitoe rai kwa wananchi tujikite kuendeleza shughuli za kiuchumi kupitia miradi midogo midogo kwa kutafuta taarifa za fursa na mikopo inayotolewa na Serikali kama asilimia 10 za Halmashauri na Wizara yetu pia" amesema Dkt. Chaula.
Ameongeza kwamba, Serikali imedhamiria wananchi wote wapate Maendeleo ili kuhakikisha Ukatili unakoma,
Kwa sasa Serikali imeandaa mwongozo wa Taifa wa kuhamasishana kusimamia Maendeleo ngazi ya msingi 2022/23-2025/26 utakaowezesha wananchi kupanga na kuamua Maendeleo yao wenyewe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TOA ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amesema malengo ya mafunzo hayo ni kupata uelewa wa namna ya kugatua madaraka kutokana na mafunzo yaliyotolewa kwa baadhi ya viongozi nchini Japani.
"Japani walianza muda mrefu na wamekuwa na mafanikio makubwa katika kuwawezesha wananchi wao kuibua miradi, upangaji wa mipango na ufuatiliaji kuanzia ngazi ya chini" amesema Msovela.
Ameongeza pia, suala la kuwashirikisha wananchi linaimarisha mahusiano mazuri ya Serikali na wananchi na kubadilisha fikra kuwa Serikali lazima ilete Maendeleo badala ya wananchi kujiletea Maendeleo yao wenyewe.
Akizungumza wakati wa Kikao hicho Mkurugenzi msaidizi wa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Stephen Mwatambi amesema ni faraja kubwa kwa nchi kuona viongozi waliopata mafunzo wanakuwa chachu ya kuendeleza waliyojifunza kwa manufaa ya wananchi.
0 Comments