HOTUBA YA KINANA KWA WAJUMBE MKUTANO MKUU MAALUM CCM YAWA GUMZO, ATAJA ATAKAYOANZA NAYO

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrhaman Kinana amepata fursa ya kuelezwa masuala mbalimbali atakayoanza nayo baada ya kupitishwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Rais Samia Suluhu Hassan.


Kinana amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi upande wa Tanzania Bara baada ya kupitishwa kwa kura zote 1875 ambazo zimepigwa na wajumbe wa mkutano huo waliokutana leo Aprili 1,2022 Mjini Dodoma.

Akizungumza mbele ya wajumbe hao wa Mkutano Mkuu wakiongozwa na Rais Samia, Kinana amesema kwamba kabla ya jina lake kupelekwa Kamati Kuu na kisha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, aliitwa na Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na walizungumza kwa saa mbili.

"Niilitwa na Rais ,nikaenda na nilipofika nikamwambia niko tayari kwa kusikiliza, mazungumzo yalichukua zaidi ya saa mbili,alinieleza mambo ya Chama, alinieleza mambo ya Serikali.Nitajitahidi kufanya kazi ya Makamu Mwenyekiti kwa bidii kwa lugha nyingine niseme sitakuangusha Mwenyekiti wetu.

"Nawashukuru Kamati Kuu kwa kupitisha jina langu, Halmashauri Kuu nashukuru lakini nawashukuru ninyi wajumbe wa mkutano Mkuu kwa kunipa kura zote,.kunipa kura zote mmenitishwa mzigo, mmenipa imani na imani huzaa amani.Pia shukrani zangu nazipeleka kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama chetu mzee Mangula.

"Mimi ni mwanafunzi wa mzee Mangula akiwa Chuo cha Kivukoni nilikuwa mwanafunzi wake , nimekuwa na Mangula kwenye vikao vya Chama, akiwa Makamu Mwenyekiti kiti wa CCM mimi nilikuwa Katibu Mkuu.Nakushukuru kwa mafunzo na maelekezo yako kwangu,"amesema Kinana.

Aidha Kinana amesema anawashukuru viongozi wote ambao amefanya nao kazi tangu Awamu ya kwanza hadi Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia na kwamba sifa zote zimetokana na viongozi hao na mapungufu aliyonayo ni yake mwenyewe

Kuhusu kazi atakayoanza k nafasi hiyo amesema kwanza atahakikisha Chama kinaendelea kuwa imara,kinachokubalika na ili kiwe imara lazima demokrasia iwe imara lazima wasimamie haki."Haki hiyo iwe ni haki ya kuchagua,haki ya kuchaguliwa bila upendeleo,bila rushwa,bila umaarufu.

"Haki ya pili ni ya kutoa mawazo, lazima wanachama wawe huru kutoa mawazo,hakuna haki miliki ya kutoa mawazo, hivyo tutamsikiliza kila mwanachama,kila mwananchi, hata kama maamuzi yametolewa hukuyapenda sikiliza kisha jenga hoja .Lazima tuheshimu demokrasia kama alichaguliwa mtu na wanachama kwanini tumpinge, tuilinde haki ya kuchagua na kuchaguliwa,

"Rais nimefuatilia mara nyingi sana akizungumzia haki, hata wakati anapokea ripoti ya mkaguzi mkuu akizungumza haki.Lazima tuwe mfano wa kusimamia haki na kukataa dhuluma,"amesema Kinana.

Aidha amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zote zinatokana na CCM, hivyo CCM si mali ya Serikalini ila serikali hizo ni za CCM.Hivyo CCM haipokei maagizo kutoka Serikalini ila CCM inaagiza Serikali kupitia Ilani na ahadi za wagombea wake na hata wanaokwenda kugombea ni CCM sio Serikali.

"Hivyo Serikali msitunyang'anye hiyo haki ya kusimamia Ilani,sera na ahadi, Serikali inapofanya vizuri na kupewa sifa, wana CCM wanayo nafasi ya kusifia na pale Serikali inapokosea wana CCM wanayo haki ya kukosa lakini kwa kutumia vikao.

"Kwa hiyo kwa maoni yangu Mzee Mkapa alisema semeni CCM pale mambo mbalimbali yanapotekelezwa na bahati mbaya siku hizi haisemwi CCM , hivyo ni wajibu wa CCM kusema yanayofanywa na tuisimamie Serikali na leo nimesoma mabadiliko ya Katiba inasema kutakuwa na vikao kila baada ya miezi sita,hapo ndipo itakuwa sehemu ya kutathimini utekelezaji wa Ilani

"Chama hili kina historia, Chama hiki kinakubalika upende usipende,lazima tuhakikishe Chama kinabakia kuwa sikio,Chama hiki kitembelee wananchi kwenye maeneo yao, tuwe sikio lao, tukifanya hivyo wataendelea kutuchagua,"amefafanua Kinana.

Ameongeza kuwa atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba inayoeleza wazi atafanya kazi kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa Chama hivyo hata akifanya ziara kwa wanananchi katika maeneo mbalimbali wajue atakua amepata baraka za Mwenyekiti wake.

Pamoja na hayo,Kinana amemshukuru Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na nafasi hiyo inafanya kuingia kwenye utamaduni wa viongozi wengine waliowahi kuwa Makatibu Wakuu wa Chama na baadae kuwa Makamu Mwenyekiti.

Mbali ya shukrani,Kinana amezungumzia umuhimu wa Umoja ndani ya Chama hicho ambacho ni kikubwa na kinapendwa na kwamba CCM haina haina mwenyewe bali ni ya watu wote, haina Ukanda.

"Nitasimamia hilo,mtu akikosa hoja,akikosa maarifa anakimbilia kwenye kichaka cha ukanda, ukabila na udini.Huo sio utamaduni wa Chama hiki, tunaweza kutofautiana kwa hoja lakini sio kwa kuleta mambo ukanda,"amesisitiza.

 Na Said Mwishehe.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments