ALIYOYASEMA SHAKA BAADA YA KUPOKEA LUNDO LA MALALAMIKO SEKONDARI CHIDYA, ATAKA WATENDAJI KUTANGULIZA UTU

 Katibu  wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka ametembelea Shule ya Sekondari Chidya iliyopo wilayani Masasi mkoani Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine amewataka watendaji wa halmashauri za wilaya na mikoa kutanguliza utu na ubinadamu kwa lengo la kuharakisha kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi.


Shaka baada ya kutembelea Shule hiyo na kupata nafasi ya kusikiliza wanafunzi amepokea malalamiko kadhaa ambayo yamekuwa changamoto na baadhi ya malalamiko ni kufuata maji umbali mrefu kutokana na mota ya shule kuungua lakini maji hayo sio safi na salama.

Katika Shule ambayo pia kuna wanafunzi wenye mahitaji Maalum ,Shaka amepokea changamoto ya gari ya shule kuharibika na hivyo wanafunzi kukosa usafiri hata inapotokea Kuna mmojawapo anaumwa lakini pia hawana daktari baada ya aliyekuwepo kuondoka.

Pia wanafunzi hao wameelezea changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara na hivyo kuwa kwenye wakati mgumu na inapofika msimu wa mvua inapita kwa shida ,hivyo wametoa ombi kwa Shaka kuangalia namna ya kuipigania ili itengenezwe.

Hivyo baada ya kupokea kero hizo Shaka ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa serikali ya Wilaya ya Masasi na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla kuchukua hatua za haraka kuondoa changamoto hizo.

Akizungumzia changamoto ya maji Shaka amesema anazo taarifa mbali na kuyafuata umbali mrefu, maji hayo kuwa machafu yamesababisha wanafunzi wengi kusumbuliwa na tatizo la kuhara, hivyo ameagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa kupeleka dawa za kusafisha maji.

Kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara Shaka ametoa maelekezo kwa Serikali ya Mkoa wa Mtwara kupitia wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kuhakisha inaifanyia matengenezo barabara inayokwenda shuleni hapo.

Wakati kwenye changamoto ya gari ya shule kuharibika ametaka kufanyika kwa jitihada za makusudi kulitengeneza ili litoe huduma zikiwemo zinazohitajika kwa dharura hususan pale mwanafunzi anapougua.

Pia, ameagiza Halmashauri kuhakikisha inapeleka shuleni hapo daktari kwa ajili kuwatibu na kuwahudumia wanafunzi hao pale wanapopatwa na changamoto za kiafya.

"Nimelazimika kusimama hapa kwa sababu nimepewa salamu zenu na mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anawasalimieni sana. Anafahamu kwamba kuna Chidya na wito wake endeleeni kufanya vizuri. Anatumia fedha nyingi sana kuwekeza kwenye elimu yenu, ndio mnana mtaona anatumia fedha nyingi kwa ujenzi wa madarasa.

"Ukweli ni kwamba Mazingira ya hapa shuleni lazima tuyaangalie , kwa mfano nimeenda kule kwenye chanzo cha maji hali ni mbaya , yale maji sio safi na salama ,tuangalie haya Mazingira, watendaji na viongozi tuwe na utu,utu,utu, tutatue changamoto hizi, hata kama ingekuwa sisi mmoja wetu akiambiwa anywe maji yale hawezi kunywa,"amesema Shaka .

Aidha Shaka ameahidi kutoa baiskeli tano za kuwasaidia wenye mahitaji maalumu, baada ya kupokea ombi kutoka kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo, Saidi Mwanyaba aliyeeleza wanauhitaji mkubwa wa baiskeli ambazo zitakuwa msaada wao kutumia kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Marko Gaguti ameelezea mbele ya Shaka kwamba maagizo yote yaliyotolewa ili kuondoa changamoto hizo yatatekelezwa haraka na akiwa shuleni hapo alitoa taarifa ya kwamba kesho dawa ya kusafisha maji itakuwa imefika, wakati changamoto ya gari nayo ameahidi kuifanyia kazi haraka.

Kuhusu changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ameahidi kuifanyia kazi kupitia TARURA.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akiwasalimia wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaosoma katika Shule ya Sekondari Chidya, aliposimama kusalimia wanafunzi akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments