Wakufunzi Wa Tehama Wa Sensa Wameaswa Kuwa Wazalendo -Kamisaa Wa Sensa Makinda

Kamisaa wa Sensa , Spika Mstaafu Anne Makinda akizungumza wakati uzinduzi wa mafunzo ya Wakufunzi wa Tehama ngazi ya Taifa na Mikoa kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya NBS Dk.Amina Msengwa akizungumza wakati kuhusiana na umuhimu wa mafunzo hayo katika kutumia  teknolojia katika ukusanyaji wa Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2022 jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wakufunzi wakiwa katika mafunzo kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, jijini Dar es Salaam.



Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022  , Spika Mtaafu Anne Makinda akiwa katika picha mbalimbali za makundi mara baada ya kuzindua mafunzo kwa wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi jijini Dar es Salaam.


*Sensa ya mwaka huu ni ya kisasa kwani inahusisha Teknolojia katika ukusanyaji wa taarifa

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
WAKUFUNZI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ngazi ya Taifa, wametakiwa kuwa wazalendo na waaminifu kwa kutunza siri wakati wa kukusanya taarifa za sensa kutoka kwa wananchi.

Hayo yamesemwa jana na Kamisaa wa Sensa nchini, Spika Mstaafu, Anne Makinda wakati wa mafunzo kwa wakufunzi 80 kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu yaliyofanyika katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Dar Es Salaam.

Alisema kumekuwa na tabia ya vijana wengi kutokuwa waaminifu hivyo, kutoa siri za nchi jambo ambalo hawalitegemei kutoka kwa wakufunzi hao.

Makinda alisema wanatarajia matokeo chanya hivyo, wanatarajia watakuwa wazalendo na si kujali maslahi kwani yatapunguza utendaji kazi wao.

"Matumizi ya teknolojia yanasaidia kuondokana na mfumo wa zamani wa makaratasi kuhesabu watu. Baada ya mafunzo haya mtakwenda kufundisha ngazi za Mikoa hivyo, tunatarajia ubora na usimamizi wa mafunzo haya ili kuondoa changamoto zitakazojitokeza," alifafanua Makinda.

Makinda aliwataka vijana hao kuonesha ewezo wao wa kusimamia kazi hiyo kwa ufanisi na kutoa matokeo kwa wakati na ubora.

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alisema sensa hiyo ni ya aina yake ambayo itatumia mfumo Tehama.

"Ili kufanikisha sensa hii tutaweza kubadilisha na kuleta maendeleo ya Taifa kupitia matumizi ya mfumo wa Tehama,"alisema Balozi Hamza.

Alisema wana jukumu la kufanikisha sensa kutokana na nafasi waliyonayo na kwamba wakikosea kuwafundisha wengine matarajio yaliyokuwa yakitegemewa na serikali hayatafikiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NBS, Dk.Amina Msengwa aliishukuru serikali kwa uendelea kuwajali wananchi wake na Benki ya Dunia kwa kuendelea kuthamini kazi ya takwimu.

Alisema matarajio yao ni ifikapo Oktoba mwaka huu wakufunzi hao wawe wameingiza madodoso kwenye mfumo huo ili kutoa takwimu za awali za sensa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments