RIPOTI MAALUMU: Malori yanavyoweka rehani roho za watu


 Ajali ya kugonganana uso kwa uso kati ya lori aina ya Fuso na basi dogo la Toyota Coaster iliyosababisha vifo vya watu 20 mkoani Tanga, imeibua siri nzito ya namna baadhi ya madereva wa malori hayo, wanavyoyaweka rehani maisha ya watumiaji wengine wa barabara.

Ajali hiyo ilitokea saa 4:30 usiku wa kuamkia Februari 4 mwaka huu wilayani Korogwe na kugharimu maisha ya watu 20 waliokuwa wakisafirisha mwili wa mpendwa wao, Atanas Mrema kutoka Dar es Salaam kwenda Rombo, Kilimanjaro ambapo wanafamilia 14 walipoteza maisha.

Uchunguzi wa gazeti la Mwananchi umebaini baadhi ya malori ya kubeba karoti, nyanya, ndizi na viazi kutoka mikoa ya kaskazini kwenda Dar es Salaam, hutumia kati ya saa saba na nane kufika jijini humo.


Kwa umbali wa kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam umbali wa takribani kilometa 620 na Moshi kwenda Dar es Salaam umbali wa kilometa 550, endapo malori hayo yangeheshimu alama za barabarani, yanapoanza safari saa za jioni yangefika asubuhi lakini yanafika usiku wa manane.

Kulingana na uchunguzi huo, licha ya malori hayo kwenda mwendo mkali na hatarishi, yakiendeshwa na vijana wenye umri kati ya miaka 28 na 35 ambao baadhi yao hutumia vilevi na mirungi wakiamini inawaondolea usingizi.

Malori yanayobeba viazi mviringo huanzia safari zake Oldonyosambo wilayani Arumeru na mengine Sanyajuu wilayani Siha huku yanazobeba karoti yakianzia safari eneo la Bonite baada ya kusafisha karoti hizo.

Mbali na bidhaa hizo, malori ya aina hiyo huanzia Mwika na Rombo yakiwa yamebeba ndizi na maparachichi na yote huanza safari nyakati za saa 1 jioni.

Uchunguzi huo umebaini, ukiacha mwendo kasi na matumizi ya vilevi, imebainika madereva huendesha malori hayo wakiwa wamewasha taa kali (full light) na mengine zikiongozewa taa za ziada ambazo ni hatarishi kwa watumiaji wengine wa barabara.


Wamiliki na madereva wa magari madogo na mabasi aina ya Toyota Coaster yanayosafiri kati ya Arusha-Moshi hadi Dar es Salaam, wanadai kuna wakati hulazimika kutoka nje ya barabara kunusuru maisha yao na abiria wao.

Hii inatokana na uendeshaji wa hatari wa baadhi ya lori ambao huwa wamewekeana dau na baadhi ya matajiri wao, kuwa endapo watafika kabla ya saa 7 usiku au 8 usiku na kugeuza kurudi Moshi au Arusha wanapewa Sh50,000.

Wakizungumza na gazeti hili, madereva hao walidai endapo askari wa Usalama Barabarani wangekuwa makini na kuwapima vilevi madereva wa malori katika vituo vya ukaguzi, wengi wangekamatwa.

Kwa mujibu wa Dk Kareem Segumba, mkufunzi mwandamizi katika Taasisi ya Afya Manyara, kiasi chochote cha pombe ambacho dereva hunywa, kinaweza kuathiri uamuzi wake pale mazingira yanapomtaka kufanya hivyo barabarani.

“Kwa sababu ukitumia kilevi chochote iwe pombe, bangi, ugoro au mirungi kinachangia ushawishi wa dereva hasa vijana kwenda mwendo kasi. Hii pia, kama ameamka na hangover (mning’inio) hawezi kuwa sawa,” alisema Dk Segumba.


Operesheni maalumu

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema mara baada ya Korogwe mkoani Tanga, walifanya operesheni maalumu kudhibiti ajali za malori, mabasi, trekta na magari mengine.

Operesheni hiyo ilianza Februari 8, mwaka huu na hadi sasa magari 103 yamekamatwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo ubovu, ‘kuovateki’ vibaya, kuzidisha abiria na utumiaji wa taa kubwa zenye mwanga mkali.

Kamanda Maigwa alisema njia zote za kuingia barabara kuu ya Arusha- Moshi hadi Tanga, kuna operesheni zinaendelea na wanaorudia kufanya makosa watafungiwa leseni na wanaoendesha wakiwa wamelewa watashitakiwa.

Alisema Jeshi la Polisi liko kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa maisha ya abiria pamoja na vyombo wanavyoendesha na kuwa wale wote waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ya barabarani watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Februari 9 mwaka huu tulianza operesheni na tulikamata magari 32, magari yenye spotlight na magari ya ‘hakuna kulala’ (Coaster zinazosafirisha abiria usiku) ambayo yalitozwa faini na kuwakamata waliokutwa na ulevi wakati wakiendesha magari,” alisema.

“Baada ya kukamata magari haya tumechukua hatua mbalimbali ikiwemo faini, magari yaliyokuwa na ubovu uliokithiri yalizuiwa kuingia barabarani hadi yatakaporekebishwa, wote hawa tutashughulika nao kwa mujibu wa sheria,” alisema.


Tatizo wamiliki

Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA) mkoa Kilimanjaro, Khalid Shekoloa alisema kuna ushawishi mbaya hufanywa na wamiliki wa mzigo hasa wanaobeba karoti kutaka dereva awahi kufika Dar.

“Kuna kikundi fulani pale mtoni Bonite unakuta mwenye mzigo ndiye anamwambia dereva wa lori ukiweza kufika Dar saa nane usiku nakupa Sh50,000 au madereva kwa madereva wana bet (wanawekeana dau) la nani atawahi Dar,” alisema.

“Kunahitajika usimamizi makini sana hiya malori yanalalamikiwa sana huko barabarani, wadereva wanajiona wao ndio wafalme wa barabara. Halafu wengi ni vijana wadogo na baadhi ni watumiaji wa vilevi,” alieleza.

Mwenyekiti wa wasafirishaji mikoa ya Kanda ya Kaskazini (Akiboa), Hussein Mrindoko alipoulizwa juu ya malori yakiwemo Fusso, canter na mengine, alisema “kwa kweli yale yanaendeshwa na vijana yanatupa shida sana barabarani. Ni janga lingine.”

“Hakuna trafiki hajui hili tatizo la hhaya malori. Mimi nashauri yawekewe mfumo wa kudhibiti mwendo na madereva wawe wanapimwa vilevi katika hizi checkpoint) wasing’ang’ane na Coaster za usiku pekee,” alisisitiza.


Madereva watia neno

Dereva wa mabasi madogo aina ya Coaster kutoka kampuni ya Special Hire, Michael Cosmas aliiomba Serikali idhibiti madereva wa malori, hasa Fusso, kwa kuwa baadhi yao wanaendesha mwendo wa hatari.

Dereva mwingine wa Coaster, Erick Ngowi alisema ni muhimu malori hayo yakafungiwa vidhibiti mwendo huku akidokeza kuwa wapo baadhi ya wateja wenye mizigo ambao huwanunua hadi pombe ili wakimbie.

Emily Bryson, mmoja wa madereva wa malori aina ya Fuso, alisema ni kweli wapo wenzao ambao hawana weledi katika kazi yao.

“Hili jambo nafikiri Serikali ingekaa na wadau wote wajadili kuhusu haya malori. Mie sina shida hata wakiweka VTS (kidhibiti mwendo) sina tatizo kwa sababu ni kwa ajili ya usalama wetu pia na watumiaji wengine wa barabara,” alisema.

Chanzo Mwananch

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments