Dk Biteko atoa maelekezo Tume ya Mipango

ARUSHA; Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameagiza Tume ya Mipango nchini kuweka uratibu wa ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi na wadau wengine katika kutoa maoni kwenye mchakato unaoendelea wa uandaaji Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

Amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa Majaliwa, katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Wanamipango 2023 iliyofanyika Novemba 27, 2023 jijini Arusha.

“Tume ya Mipango hakikisheni wananchi wote wanashiriki kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Tanzania wanayoitaka katika miaka 25 ijayo, maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050  yameanza na kutokana na umuhimu wa Dira kwa taifa letu, wanamipango na wadau wote ni muhimu kila mmoja  kwa nafasi yake ashiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi kama atakavyohitajika.” Amesema Dk. Biteko

Aidha amewasisitiza Maafisa Mipango kubadilika na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya Miradi na Programu zote zinazotekelezwa katika maeneo yao ikiwemo zinazofadhiliwa na Wadau wa Maendeleo badala ya ile inayogharamiwa na Serikali Kuu au halmashauri pekee.

Pia, Dk.Biteko ameelekeza Wakurugenzi wa Mipango kuzingatia utamaduni wa kuwa na mawazo ya pamoja katika kupanga mipango ya serikali na nchi kwa ujumla ili kuleta mipango imara itakayosaidia taifa kufikia uchumi wa juu.

Suala jingine alilosisitiza Dk. Biteko ni Wanamipango waliopewa jukumu la kusimamia miradi pamoja na ufuatiliaji na tathmini kuzingatia utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa.

Sanjari na hayo, Dk. Biteko amesema kuwa, Shughuli za tathmini na ufuatiliaji ni muhimu nchini hivyo zinapaswa kupewa kipaumbele cha kutengewa rasilimali za kutosha.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa,  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments