Watu saba wamefariki dunia na wengine 24 kulazwa katika Hospitali ya Wilaya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya kula kitoweo cha samaki aina ya kasa anayedaiwa kuwa na sumu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi Khamis amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 25, 2021 mwaka huu eneo la Soko la Msuka na Tumbe katika Wilaya ya Micheweni.
Amesema watu hao baada ya kula samaki huyo walianza kutapika na kuharisha ndipo walipelekwa kupata matibabu hospitalini.
"Siku hiyo ya tarehe 26 walikufa watu watatu, tarehe 27 wakafa wengine wawili na Jumapili wamekuwa wengine wawili, hivyo kufikia idadi ya watu saba walifariki dunia kutokana na tukio hilo," amesema
Amesema watu 16 kati ya 24 waliokuwa wamelazwa wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya afya zao kuimarika huku wengine wanane wakiendelea kupata matibabu.
"Huyo samaki yeye mwenyewe anasumu kama ukimkosea kumpika bila kuondoa sumu yote lakini pia inawezekana walimtoa sumu ila kutokana na samaki hao kutoweka duniani kwahiyo kuna baadhi ya mataifa wanawadunga sindano za sumu wanapowafuga ili wasiliwe," amesema na kuongeza
"Kwahiyo inawezekana hata huyo alikuwa anafugwa sehemu sasa akaja kwenye ukanda huu wa kwetu wakamkamata na kumfanya kitoweo bila kujua kama ana sumu,"
0 Comments