Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia moja ya maduara yaliyofungwa kuepusha madhara kwa wachimbaji katika Kijiji cha Nsungwa wilayani Kaliua. Picha na Robert Kakwesi.
Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewahimizi wachimbaji madini wadogo kutofanya starehe za kupitiliza na kusahau kuweka akiba kwa ajili ya kufurahia maisha uzeeni.
Akizungumza na wakazi wa kitongoji cha namba tano katika Kijiji cha Nsungwa,wilayani Kaliua leo Jumanne Waziri Biteko amesema shughuli ya uchimbaji ni ngumu na wachimbaji wanapaswa kujiwekea akiba ili pale siku nguvu zinawaishia wasisumbue wengine kutunzwa.
Amewataka kufanya starehe kiasi baada ya kuingiza kipato na kulipa stahiki za Serikali kwa vile ni haki yao pia kufurahia maisha na kutumia jasho lao.
"Fanyeni starehe kidogo lakini bila kusahau kuweka akiba kwa ajili ya siku nguvu zenu zitakapoisha msije kuwasumbua wengine"Amesema
Waziri huyo ameeleza kufurahishwa na utulivu katika mgodi huo wa Nsungwa, kwamba una utulivu mkubwa na watu kufanya shughuli zao kwa amani.
Amesema kama Wizara wanataka wachimbaji wawezeshwe na hata kwenda kuchimba nje ya nchi kwani itaonesha kuwa wanatumia fursa kikamilifu.
Pia, Waziri Biteko amesisitiza wachimbaji kuwa makini kufuata maelekezo ya kutotumia maduara yalifungwa akiwataka wasijaribu kwenda kuchimba wakati wa usiku kwani ni hatari kwao.
Amesema wameona kuna hatari kubwa kwa wachimbaji kupata madhara kama wataendelea kuyatumia na ndio maana wameyafunga.
"Maeneo mengi ambayo kumetokea madhara ni kwa vile wachimbaji hawakufuata maelekezo au uamuzi uliofanywa wa kuzuia uchimbaji na wao kwenda kinyume"Amesema
0 Comments