Asimulia alivyoepuka adhabu ya kifo


 Desemba 6 ilikuwa siku mpya kwa Zacharia Mahushi (49), ambaye aliachiwa huru baada ya kukaa gerezani kwa takribani miaka 20 akisubiri adhabu yake ya kifo.

Hata hivyo, alikumbana na changamoto ya wapi aanzie maisha, kwani hakujua aende wapi, hajui ndugu na famili yake ilipo. Uhuru wake ukamwongezea sintofahamu nyingine.

Baadaye alifanikiwa kukutana na binamu yake, Daniel Mhando ambaye alimwacha akiwa mdogo na sasa ndiye anampatia hifadhi eneo la Goba.

Siku aliyoachiwa aliagana na mtuhumiwa mwenzake ambaye aliwaomba ndugu zake wampokee Mahushi kama angeachiwa huru, bahati nzuri aliachiwa na akapokewa na ndugu wawili wa mtuhumiwa huyo. Mahushi alichukuliwa na mke wa mtuhumiwa huyo mpaka nyumbani kwake, Mbweni. Alianza kuwatafuta ndugu zake, lakini aliambiwa baadhi wamefariki akiwemo baba yake, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo.

Alifanikiwa kukutana na Mhando, kijana ambaye wakati anakamatwa mwaka 2002, alikuwa mtoto mdogo na hivyo wasingeweza kutambuana bila kuunganishwa na ndugu wengine wa mikoani waliompa taarifa zake. Mahushi anasema anahitaji msaada wa kupata makazi na kazi ya kufanya, ili imsaidie kuendesha maisha yake. Yeye ni fundi wa kutengeneza paving, ujuzi alioupata akiwa gerezani.

Jana Mahushi alifanya mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi akisema maisha yake yalibadilika baada ya bosi wake kuvamiwa na kuuawa na majambazi, wakati yeye na wafanyakazi wengine katika nyumba hiyo wakishuhudia.

“Tukio lilitokea mwaka 2002 maeneo ya Mbezi Beach nikiwa kwa bosi wangu nikishughulika na kazi ya bustani katika nyumba yake. Nakumbuka siku hiyo nilipewa kazi ya kuweka dawa kwenye maua, nikishirikiana na wafanyakazi wengine.

“Bosi hakuwepo, wakati naendelea na shughuli zangu saa nne asubuhi mlango ukagongwa, nilipowauliza wanataka nini wakasema wamekuja kurekebisha umeme. Ilinibidi niwaulize wenzangu kama kuna ahadi ya mafundi, wakasema hawana habari,” anasema.

Anasema alirudi kuwaeleza watu hao kuwa hawana taarifa zao na waliondoka, lakini muda mfupi baadaye mmoja wa wasichana aliyekuwapo katika nyumba hiyo alitoka nje kutupa taka na aliporudi aliingia na watu wale. Hata hivyo, Mahushi anasema alipowasogelea alibaini hawakuwa watu wema na ghafla walianza kutoa amri iliyokuwa ikimlenga yeye moja kwa moja, ikiwemo kupigwa na kufungiwa kwenye chumba kimoja katika nyumba hiyo.

“Saa saba mchana nilisikia gari na nilipoangalia dirishani nikamuona mzee (bosi), akishuka na muda mfupi alishambuliwa na watu wale na kufariki dunia. Baada ya hapo walikuja kunitoa chumbani lakini kukawa na mabishano kwamba niuawe au la.

“Walinichukua na kunifunga kitambaa usoni, wakanipeleka nyumba ya kulala wageni eneo la Vingunguti, ingawa ilikuwa ngumu kujua kwa wakati huo. Usiku nikasikia kelele kumbe walikuwa polisi, nilipowaelezea ilikuwa ngumu kuelewa kwamba sikuhusika na tukio hilo, walinipeleka Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam,” anasema. Alikaa katika kituo hicho kwa siku tatu, kabla ya kupelekwa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kusomewa mashtka ya mauaji na kupelekwa mahabusu katika gereza la Keko, Juni 2002.

“Wakati kesi ikiendelea, kitu kilichokuwa kinaniumiza ni kuingia katika kesi ya mauaji wakati sijaua, lakini maelezo yalionekana nimeua kwa sababu ilinibidi nikiri kosa baada ya kubanwa na polisi. Mahakamani sikusema kama nimeua kwa sababu sikupata mateso,” anasema.

Anasema hadi sasa anaendelea kuwatafuta ndugu zake, wakiwamo watoto wake wawili wa kiume; Baraka na Shangwe. Anasema ameambiwa mtoto wake mmoja yuko Morogoro, lakini hajawasiliana naye.

Mahushi anasema ameamua kwenda kwenye vyombo vya habari akiamini atapata msaada wa kuunganishwa na familia yake pamoja na kupata msaada mwingine wa kibinadamu. Mwenye nia ya kumsaidia Mahushi anaweza kuwasiliana naye kupitia namba ya binamu yake, Daniel Mhando – 0712091908.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments