Na Dotto Mwaibale, Singida
JUMUIYA ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida inajivunia mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Singida Yusuph Mwandami wakati akihutubia kwenye hitimisho la maadhimisho ya sherehe ya miaka 45 ya kuzaliwa chama hicho kwa jumuiya hiyo yaliyofanyika Kata ya Kinyeto Wilaya ya Singida DC jana.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa nyumba za makatibu wa jumuiya ambazo zimejengwa kila wilaya huku zingine zikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Alisema nyumba hizo zimejengwa katika wilaya zote zikiwemo za Singida, Iramba, Manyoni na Ikungi.
Katika hatua nyingine Mwandami amewaomba wanawake nchini kuacha kuwadharau waume zao na kuwa iwapo mwanaume akija kujua na kuamua kumdharau mke wake atakuwa hamdharau mke wake pekee bali ni wote akiwepo Rais.
"Mwanaume akichukia hayawezi kuishia kwa mke wake bali atawachukia wanawake wote ni vizuri sasa kama wapo wanaofanya hivyo na wahimiza wabadilike na kuwa na heshima kwa wanaume wao" alisema Mwandami.
Alisema hivi sasa kumekuwepo na sintofahamu kuhusu kusimamia maadili katika kulea watoto kwani kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakitofautiana na kufikia hatua mmoja kati yao kudiriki kumgombeza mwenzake pale anapoonywa mtoto anapokosea tena mbele ya mtoto.
Mwandami alisema tabia hiyo imekuwa ikiwajengea kiburi watoto hivyo kuwa changamoto kubwa katika familia na kwa Taifa kwani ndio wanaotegemewa kuwa viongozi wa kesho.
Aliwaomba wazazi na walezi kuwa walezi wazuri bila ya kujali ni wake au wa mtu mwingine kama walivyokuwa wakifanya wazee wetu hapo zamani jambo litakalo saidia kupata taifa lenye maadili.
Kabla ya mkutano huo Kamati ya Utekelezaji ya Wilaya ya Singida DC pamoja na Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Singida ambaye alikuwa mgeni rasmi Yusuph Mwandami walikagua miradi mbalimbali katika kata hiyo ikiwepo ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkimbii, ujenzi wa Shule ya Msingi Ntunduu, ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa sita na ofisi moja Shule ya Sekondari Kinyeto B madarasa yalitokana kwa fedha za mradi wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 na ukaguzi wa Zahanati ya Kata hiyo.
Kamati hiyo pia ilikagua ufyatuaji wa matofari kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto ambapo pia ilifanyika harambee kwa ajili ya ujenzi wa Katibu wa jumuia hiyo ngazi ya wilaya ambapo zilipatika Sh.248,000 na mifuko ya saruji 19.
Katibu wa jumuiya hiyo wilayani humo Jumanne Mghunda alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo ambapo wilaya yao imepata zaidi ya Sh.Bilioni 2.
Aidha Mghunda aliwaomba Wana CCM wilayani humo wakati utakapo wadia wa uchaguzi ndani ya chama 2022 kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali na kuhiriki katika zoezi la Sensa ya watu na Makazi pamoja na kulipia kadi zao kwa kutumia mfumo wa kielekitroniki.
Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa wilaya wa jumuiya hiyo, Alex Mbogho alimshuru mgeni rasmi Mwandami kwa kukubali kuhudhuria mkutano huo na kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo hasa ujenzi wa ofisi za jumuiya hiyo na nyumba ya katibu wazazi wilayani humo.
Katika mkutano huo wananchi 50 walijiunga na chama hicho huku saba wakitokea vyama vya upinzani.
0 Comments