Kiongozi wa Mali, Kanali Assimi Goita amesema kuwa, vikwazo hivyo ambavyo ni pamoja na nchi yake kufungiwa mipaka na kuzuiwa kufanya biashara, vinawatesa wananchi.
Aidha Mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Mali ameeleza kuwa, atakuja na mpango wa kuhakikisha kuwa, uhuru wa nchi yake unalindwa baada ya kuwekewa vikwazo.
Kadhalika amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) baada ya jumuiya hiyo kuiwekea vikwazo vikali nchi yake kutokana na serikali ya mpito kushindwa kuitisha uchaguzi mwezi ujao wa Februari mwaka huu kama ilivyopangwa hapo awali.
Haya yanajiri baada ya kundi la ECOWAS siku ya Jumapili, kuweka msururu wa vikwazo dhidi ya Mali, kutokana na serikali ya mpito kuakhirisha uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi ujao wa Februari. Serikali ya muda ya Mali imeakhirisha uchaguzi huo hadi Disemba mwaka 2025.
Nchi wanachama wa ECOWAS zimeamua kusimamisha biashara na Mali isipokuwa bidhaa za kimsingi, kukata misaada ya kifedha, na kufunga akaunti ya Mali katika Benki Kuu ya Mataifa ya Afrika Magharibi.
0 Comments