Na Dotto Mwaibale, Singida
WAJASIRIAMALI wa Soko la Samaki Samaki lililopo Kata ya Mandewa mkoani hapa wameuvunja uongozi wa soko hilo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye mkutano ulioitishwa na Diwani wa kata hiyo Baraka Hamisi kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali za wajasiriamali hao waliohamishwa kutoka katika maeneo yasio rasmi ya barabarani na kupelekwa katika soko hilo Selemani Sima alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na viongozi hao kushindwa kuweka miundombinu katika soko hilo.
"Katika soko ili hakuna miundombinu kabisa jambo linalosababisha kufanya biashara zetu kwenye mazingira hatarishi" alisema Sima.
Balozi wa Mtaa wa Unyankhae Juma Mataka aliitaja miundombinu ambayo haipo kwenye soko hilo kuwa ni choo, guba la takataka, maji, umeme na kuwa kukosekana kwa miundombinu hiyo kunatishia usalama wa afya zao.
Alitaja changamoto nyingine kubwa iliyokuwepo ni usalama wa bidhaa zao kwani kulikuwa hakuna ulinzi lakini sasa wamewapata kutoka Kampuni ya Gema ambao watakuwa wakiwalipwa Sh.300,000 kwa mwezi.
Mjasiriamali Mohamed Ngura alisema changamoto nyingine kubwa iliyo jitokeza kwenye soko hilo ni wajasiriamali wa kata hiyo walioondolewa maeneo yasiyo rasmi kukosa maeneo ya kufanyia biasharazao baada ya kupewa watu wengine kutoka nje ya kata hiyo.
"Tulivyo hamishwa kule barabarani kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyoagiza na kupangiwa na Manispaa ya Singida tuje hapa watu wengi wamekosa maeneo ya kujenga vibanda vyao kutokana na kupewa watu kutoka nje ya kata hii" alisema Ngura.
Ngura aliongeza kuwa kutokana na soko hilo kutokuwa na miundombinu kwa sababu ya viongozi wa soko hilo kushindwa kufanya kazi yao ipasavyo baadhi ya wafanyabiashara wamerudi katika maeneo ya awali waliondolewa na kufanya soko hilo kukosa wateja ambao wanawafuata wenzao maeneo ya awali.
Diwani wa Kata ya Mandewa Baraka Hamisi baada ya kupokea malalamiko ya wajasiriamali hao aliridhia viongozi wa soko hilo kusimamishwa ambapo walichaguliwa wengine wa mpito hadi hapo watakapo chaguliwa wapya mapema wiki hii.
0 Comments