Watatu wakamatwa wizi wa Sh2.12 bilioni za Selcom Iringa


Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limewakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa watatu wa wizi wa zaidi ya Sh2.12 bilioni mali ya kampuni ya Selcom Paytech Limited.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 11, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema kuwa wizi wa fedha hizo ulifanyika kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Iringa, Dar es salaam na Morogoro kati ya Novemba 9 hadi 27, 2021 baada ya wakala kufanikiwa kuchezea mfumo wa kielektroniki wa Selcom Pay unaomilikiwa na kampuni hiyo.

Bukumbi ameeleza kuwa wakala wa Selcom Pay, Tyson Kasisi (ambaye ni mtuhumiwa) wa mkoani Iringa kupitia huduma hiyo isivyo kihalali alihamisha fedha kwenda namba mbalimbali za simu na kisha kuchukua fedha hizo kupitia mawakala mbalimbali wa huduma za kifedha za mtandao pamoja na kaunti za benki.

“Wakala huyo kwa njia ya udanganyifu alianza kujitumia fedha pamoja na kuwatumia watu wengine kwa kushirikiana na genge lake la uhalifu walifanikiwa kuiba zaidi ya Sh2.12 bilioni,” amesema Bukumbi

Amesema Jeshi hilo limefanikiwa kuokoa fedha taslimu zaidi ya Sh956.97 milioni kutoka kwa watuhumiwa wa washirika wa uhalifu huo ambao walipokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuzificha katika maeneo mbalimbali ikiwamo makazi na shambani.

Pia amesema zaidi ya Sh121.21 milioni zimezuiliwa katika moja ya benki za biashara mkoani Iringa ikiwa ni mazalia ya uhalifu huo, huku akiwataja watuhumiwa kuwa pamoja na Tyson Kasisi, Patrick Chalamila na Evaristo Chalamila. 

Bukumbi amesema kuwa mali ambazo ni mazalia ya uhalifu zimekamatwa na kuhifadhiwa ikiwa ni magari manne yenye thamani ya Sh303 milioni.

Ametaja mali hizo kuwa pamoja na gari aina ya Scania yenye jina la mtuhumiwa Patrick Chalamila lenye thamani ya zaidi ya Sh128 milioni, Mistubish Fuso lenye jina mtuhumiwa Tyson Kasisi likiwa na thamani ya zaidi ya Sh75 milioni.

Mengine ni pamoja na Toyota Harrier lenye jina mtuhumiwa Tyson Kasisi kwa thamani ya zaidi ya Sh72 milioni na Nissan Juke lenye jina la mtuhumiwa Patrick Chalamila na lenye thamani ya zaidi ya Sh28 milioni.

Pia tumekamata gari Toyota IST mali ya Patrick Chalamila lililokuwa linatumika kufanikisha uhalifu kwa kusafirisha fedha za wizi kutoka Madibira Wilaya ya Mbarali na Ilula wilayani Kilolo kwenda kuzificha Kilombero Mkoani Morogoro,” amesema Kamanda Bukumbi.

Amesema wamekusanya ushahidi wa kutosha na kuwafikisha watuhumiwa 10 mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ikiwa pamoja na kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments