Kingu ameyasema hayo leo Jumanne Mei 9, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2022/2023.
Amesema ukienda kwenye vyuo vya nchi za Uganda na Kenya utakuta Watanzania wengi wanasoma kwenye vyuo hivyo kuliko wale wanaokuja kusoma nchini Tanzania.
“Nenda kaangalie idadi ya wanafunzi wanaoenda kusoma nchini Kenya, nenda kaangalie idadi ya wanafunzi waookuja kusoma hapa nchini utakuta kuna mwanya mkubwa,”amesema.
Amesema na sababu kubwa ya idadi ndogo ya watu kutoka nje ya nchi kusoma hapa nchini ni urasimu wa kungangania vitu ambavyo havilifungui Taifa kielimu.
Ameshauri Serikali kulifungua Taifa kwasababu litafanya Tanzania kuchangamana kielimu na kuvuta teknolojia ambayo itasaidia katika kuendeleza nchi kiteknolojia.
Ametoa mfano wa Tanzania imeweka sharti ya mtu ili aweze kuingia chuo kikuu kusoma shahada anatakiwa awe amemaliza kidato cha sita lakini Kenya mtoto akifika kidato cha nne anajiunga na masomo ya shahada.
Hata hivyo, amesema mwanafunzi huyo alimaliza kidato cha nne akija hapa nchini anakataliwa kusoma masomo ya shahada.
Ametaja faida zitakazotokana na kufungua udahili wa wanafunzi kutoka nje ya nchi kutaongeza mapato kwa vyuo vikuu, kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia kutoka nchi nyingine na itasaidia kujenga mshikamano wa kikanda.
Aidha, amesema Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 imempa madaraka Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuunda Baraza la Ushauri wa elimu.
Hata hivyo, amesema hadi kufikia sasa baraza hilo halijaundwa na hivyo kumtaka Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda kwenda kuliunda.
Amesema kwa kuliunda baraza hilo kutasaidia kuondoa kelele za wabunge.
0 Comments