Mwelekeo mpya uteuzi wa Mkuu wa Magereza

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteuwa Mzee Ramadhan Nyamka kuwa Kamishna wa Magereza akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Suleiman Mzee ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Uteuzi wa Nyamka umeonyesha mwelekeo mpya katika teuzi za wakuu wa chombo hicho kinachorekebisha nidhamu za wahalifu, ambapo miaka ya karibuni waliteuliwa kutoka nje ya jeshi hilo.

Nyamka amepandishwa kutoka Kaimu Kamishna wa Magereza Huduma za Urekebu, kinyume na mtangulizi wake Brigedia Jenerali Suleiman Mzee aliyetokea Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Brigedia Jenerali Mzee aliteuliwa na Hayati John Pombe Magufuli, Januari 31, 2020 akitokea jeshini, ikiwa ni siku chache tangu mkuu wa nchi wa wakati huo akosoe utendaji wa magereza.

Dalili za Hayati Magufuli kuteuwa mkuu wa Magereza kutoka JWTZ zilianza kuonekana tangu Machi 16, 2019 alipofanya ziara ya kushtukiza na kukuta ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo Ukonga, uliokuwa ukifanywa na Wakala wa Majengo (TBA) ukisuasua.

Kutokana na hali hiyo Hayati Magufuli aliagiza mradi huo ukabidhiwe kwa JKT na kuwataka wataalamu wa TBA na askari Magereza kulipisha jeshi hilo lililojenga Ukuta wa Mirerani na nyumba 45 za Serikali Dodoma.

Alipokuwa akikabidhi ujenzi huo kwa JKT Magufuli alisema: “Siku tutawakabidhi Magereza nyumba zilizojengwa na jeshi, inawezekana siku moja wakaanza kujifunza kuona aibu, lakini siku moja wasije wakashangaa nikimteua mkuu wa magereza akawa mwanajeshi.

“Ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnaakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofali, tuanze kujenga,” alisema Hayati Magufuli.

Hata hivyo, kabla ya Mzee aliyekuwa Mkuu wa jeshi hilo ni Phaustine Kasike aliyeteuliwa kutoka Magereza.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments