Miili hiyo ambayo ilitarajiwa kuwasili jana Jumapili saa nne usiku ikitokea mkoani Tanga na kupumzishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya leo siku ya Jumatatu ambapo ndugu jamaa na marafiki wataaga wapendwa wao katika viwanja vya hospitali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea Februari 4, katika eneo la Magira Gereza, Kata ya Magira Gereza, wilayani Korogwe, Barabara ya Segera - Buiko na kusababisha vifo vya watu 20 mpaka sasa.
Ndugu hao pamoja na majirani walikuwa wakisindikiza mwili wa ndugu yao, Athanas Mrema (59) aliyefariki dunia Februari Mosi, kutokea jijini Dar es Salaam kuja mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko ndipo walipokutana na ajali hiyo mbaya.
Akizungumzia taratibu za kuaga miili hiyo kesho, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amesema mipango ya mazishi inaendelea vizuri na kwamba katika wilaya hiyo watapokea miili 16 ikitokea Tanga ambapo 14 ni ya familia moja.
Amesema miili hiyo itaanza kuagwa saa mbili asubuhi kesho Februari 6 ambapo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ataongoza mazishi hayo kwa kushirikina na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.
Amesema wilaya hiyo imeandaa magari 13 kwa ajili ya kubeba miili hiyo na yatakwenda kwa Eskoti ya Jeshi la polisi kufikisha miili kwenye familia ambazo zimepoteza wapendwa wao.
Akizingumza kwa niaba ya ukoo wa Mrema, Colman Mrema amesema tayari wameshaandaa maeneo ya maziko kwa ajili ya kuzika miili ya ndugu zao.
Baadhi ya miili itazikwa katika Kitongoji cha Kirungu Mokala, Kata ya Kelamfua Mokala, Keryo, Mengwe na Shimbi wilayani humo.
Chazo Mwananchi
0 Comments