Tatizo la ukosefu wa uadilifu miongini mwa baadhi ya viongozi wa Umma linadaiwa kusababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo ubinafsi kwa viongozi hao.
Hayo yamesemwa mjini Butiama leo Aprili 16, 2023 na washiriki wa mdahalo wa kumbukizi ya Mwalimu Nyerere wakidai kuwa umefika muda sasa viongozi wa Umma kujifunza na kuishi misingi iliyoongoza maisha ya mwalimu Nyerere.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) iliyoandaa mdahalo huo, Joseph Butiku amesema viongozi wanaofanya ubadhirifu wa mali za umma wanafanya hivyo makusudi kwani wana miongozo inayowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Ni ubinfasi tu kwasababu viongozi wanaofanya ubadhirifu ni ama wameapa au wana miongozo ya namna ya kutimiza wajibu wao kwahiyo hicho wanachokifanya wanajua madhara yake lakini kwasababu wametanguliza mbele ubinafsi wala hawaoni shida,”amesema
Amesema kuporomoka maadili kwa viongozi kwa namna moja ama nyingine kunachangia kuporomoka kwa maadili katika jamii kwasababu viongozi wanatumika kama kioo cha jamii kujifunza.
“Jamii inawachukulia viongozi kama kioo sasa kama wao wanajilimbikizia mali na kutanguliza rushwa kwa vyovyote pia jamii itaiga hayo hayo kwasababu itaona kuwa hiyo ndiyo njia rahisi ya kufanikiwa,” amesema
Kada wa CCM, Stephen Wasira amesema viongozi wanapaswa kujifunza kwa hayati Baba wa Taifa ambaye muda wake wote wa uongozi alikuwa kiongozi mtumishi na sio mtawala.
“Mwalimu alikuwa kiongozi mtumishi na sio bwana mtawala hakuwa na majivuno lakini kubwa zaidi alikuwa mzalendo na sisi tunapaswa kutembea humo humo kwa maslahi ya nchi yetu,” amesema Wasira
Katibu Mstaafu wa CCM, Wilson Mkama amesema hayati Mwalimu Nyerere alikuwa tayari kutumia muda wake wote kutafuta majawabu ya changamoto za binadamu na sio kujilimbikizia mali.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa MNF, Profesa Francis Matambalya amesema kwa hali ilivyo nchini ni vigumu kumlinganisha hayati Mwalimu Nyerere na viongozi wa sasa.
“Tutakuwa hatumtendei haki mwalimu Nyerere na kizazi cha sasa kwani mwalimu pamoja na mambo yote lakini alikuwa mvumilivu sana hakuwa na tamaa lakini bado tuna nafasi ya kurekebisha haya hebu turudi kwenye mstari,”amesema
0 Comments