Dk Asha-Rose Migiro, Mtanzania aliyeweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza mwanamke kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amerejea nchini baada ya kumaliza kipindi cha miaka saba kama balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Dk Migiro ni miongoni mwa Watanzania waliofika mbali kimataifa kama Dk Salim Ahmed Salim, aliyewahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1981, baada ya aliyekuwa kwenye nafasi hiyo, Kurt Waldheim wa Austria kumaliza kipindi chake cha pili.
Dk Salim aliyeikosa nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura ya veto na Marekani, baadaye alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika kuanzia mwaka 1989 hadi 2001.
Kurejea nyumbani kwa Dk Migiro licha ya umri wake wa miaka 67, bado anaweza kurejesha uzoefu wake kulijenga Taifa.
Weledi wa kiutendaji wa Dk Migiro uliwekwa wazi na Ban Ki-moon mwaka 2007 alipomteua kuwa msaidizi wake, akisema ni kiongozi anayeheshimika, na katika miaka mingi iliyopita alikuwa amejishughulisha na maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Majukumu ya Dk Migiro kwenye nafasi hiyo yalikuwa kushughulikia usimamizi na mambo ya utawala ya ofisi ya sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na masuala ya jamii, uchumi na maendeleo. Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu alikuwa Louis Frechette wa Canada.
Kurejea kwa Dk Migiro kunaelezwa ni hazina nyingine kwa Taifa na kwenye medani za kisiasa.
Aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi aliwahi kunukuliwa akisema Dk Migiro wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliingiza maofisa wapya wizarani na kuweka malengo ya wasaidizi waandamizi wake na kuinua ufanisi wa wizara hiyo.
Pia, Dk Salim wakati huo akiwa mjumbe maalumu wa mazungumzo ya amani ya suala la Darfur wa Umoja wa Afrika, alinukuliwa akisema Dk Migiro ni mwerevu, amepata elimu bora na ana kipaji cha kuongea, hivyo yeye ni mtu mwafaka kwa wadhifa wa Naibu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Hata alipomaliza muda wake kwenye wadhifa wa naibu katibu mkuu, Ban Ki-moon alimteua kuwa mwakilishi wake maalumu wa masuala ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi barani Afrika.
Nafasi yake kisiasa
Dk Migiro aliyewahi kuomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, amewahi kuwa katibu wa halmashauri kuu ya Taifa, idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa, akiwa chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Wasemavyo wadau
Akizungumza na gazeti hili, mdau wa masuala ya siasa nchini, Nzengo Kasubi alisema licha ya umri wa miaka 67 alionao Dk Migiro, ana nafasi ya kuteuliwa kwenye baraza la mawaziri kama ilivyokuwa kwa Sir George Kahama, mpigania uhuru aliyerejeshwa kwenye uwaziri akiwa na umri wa miaka 71.
Kasubi alisema hata baraza la sasa la mawaziri lina mawaziri wenye umri wa miaka 75, 66, 63, 62, 61,60 na 59 ambao wanachapa kazi kwa weledi na umri siyo kikwazo kwao.
Alisema Sir George Kahama alikuwa mpigania uhuru wa Tanganyika na waziri wa mwanzo wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika Serikali ya Rais Julius Nyerere, na mwaka 2000 Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Ushirika akiwa na umri wa miaka 71.
Semeni Juma, ambaye ni mchumi, alisema kurejea kwa Dk Migiro kunatoa mwanga wa mabadiliko ndani ya Serikali au kwenye CCM kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu kwenye masuala ya kimataifa na siasa.
Alisema akiwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, alizunguka maeneo mengi ya nchi kukikiimarisha chama chake cha CCM, akiwa na Katibu Mkuu Kinana.
Ndani ya Sekretarieti ya CCM
Dk Migiro amekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Siasa na Uhusiano kwenye Sekretarieti iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana; Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba; Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye; Katibu wa Oganaizesheni, marehemu Mohammad Seif Khatib na Katibu wa Fedha na Uchumi, Zakia Meghji.
Sekretarieti hii ndiyo mwaka 2013 ilizunguka nchi nzima kurejesha uhai wa chama na kuwezesha kurejesha imani ikiwamo wanachama kuvaa sare za chama hicho na waliwezesha kufanikisha maadhimisho ya miaka ya 36 ya CCM yaliyofanyika mkoani Kigoma.
Nafasi za uwaziri
Dk Migiro amekuwa waziri kwa marais wawili, wakati wa Mkapa alikuwa Waziri wa Wanawake, Jinsia na Watoto, huku dada yake Mwamtumu Malale akiwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Hata hivyo, baada ya hilo kubainishwa, Rais Mkapa alitoka hadharani akisema alipofanya uteuzi hakujua waziri na katibu ni watoto wa tumbo moja, hivyo alimhamisha mmoja.
Dk Migiro pia amekuwa waziri kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, akishika nafasi za Waziri wa Katiba na Sheria; na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa wakati huo.
Kugombea urais
Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliingia kwenye tatu bora ya walioomba kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Hata hivyo, kwenye mkutano mkuu wa CCM alishindwa na Dk John Magufuli aliyepata asilimia 87.1 ya kura zote 2,104 akifuatiwa na Balozi Amina Salulm Ali aliyepata asilimia 10.5 ya kura zote ikiwa ni sawa na kura 253 na wa tatu alikuwa Dk Migiro aliyepata kura 59 sawa na asimilia tatu.
Familia yake
Gazeti hili liliwahi kuzungumza na kaka yake Ally Shaban Mtengeti, ambaye alisema Dk Migiro ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia yao.
Alisema mdogo wake huyo hana makuu na anapenda watu, lakini asiyependa kuonewa.
Mtengeti alisema mdogo wake ana nyota ya uongozi, kwa kuwa alianza kuongoza tangu akiwa chuo kikuu ambako alikuwa mbunge kwenye baraza la vyuo vikuu.
0 Comments