Dola yapaa, ikivunja rekodi, uhaba tishio

Thamani ya Dola ya Kimarekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania imefikiwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanza kutumika kwa sarafu hizo.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya soko la fedha hapa nchini, jana Dola moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,550 na ikinunuliwa kwa Sh2,510, jambo ambalo limeibua wasiwasi miongoni mwa watu, hususan wanaotumia sarafu hiyo katika manunuzi.

Tangu Oktoba mwaka jana Dola ya Kimarekani ambayo hutumiwa katika miamala ya kimataifa kwa asilimia 85 imekuwa ikiimarika dhidi ya sarafu nyingine, jambo ambalo linatajwa kusababishwa na sheria ya kupambana na mfumuko wa bei iliyopitishwa na Taifa hilo la kwanza kiuchumi duniani.

Akizungumzia mwenendo unaokuwa wa thamani ya Dola dhidi ya Shilingi, mchumi Dk Jane Buberwa anayeishi Dar es Salaam alisema litasababisha ongezeko la bei kwa watumiaji wa chini.

“Matokeo ya kinachoendelea yataanza kuonekana kwa kuongezeka kwa gharama za bidhaa ambayo itasababisha ongezeko la matumizi kwa wateja,” alisema Dk Buberwa alipozungumza na gazeti la The Citizen.

Hata hivyo, Dk Buberwa alisema hali hiyo inajitokeza si tu kwa Tanzania, bali pia kwa baadhi ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wake mhadhiri msaidizi wa masuala ya benki na sarafu za kimataifa wa Chuo Kikuu cha Ardhi, akizungumza na gazeti la The Citizen jana alisema hali hiyo itaathiri uchumi wa watu kwa sababu nchi inaagiza bidhaa nje kuliko kuzalisha ndani.

“Kama hali hii itaendelea, itasababisha mfumuko wa bei katika uagizaji wa bidhaa. Pia utasababisha ongezeko la bei za bidhaa kutokana na bei ya manunuzi nje kutegemea uimara wa Dola,” alisema.

Akizungumzia suala la Dola katika mkutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadhi ya wafanyabiashara wa fedha za kigeni jana, Deogratius Marandu, anayefanya biashara ya fedha za kigeni aliwataka Watanzania kulinda thamani ya Shilingi.


“Kuna umuhimu wa kila Mtanzania kulinda thamani ya Shilingi yetu. Tusipoilinda ikashuka thamani na kufika Sh3,000 hadi 4,000 kwa Dola moja maana yake tutakuwa tukinunua bidhaa chache kwa fedha nyingi,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema; “Kwa mfano wewe unahitaji Dola Desemba na huyu anahitaji Agosti, unapokuja kununua unamfanya huyu wa Agosti kuzikosa.

Marandu alisema kutokana na matukio ya maduka hayo kufungwa, bado kuna hofu miongoni mwa wafanyabiashara.

“Tangu Serikali ilipofunga biashara, bado watu wana hofu, ni vizuri hata polisi kututoa hofu. Gavana alituita akatuambia tuko kwa ajili ya biashara na anapitia upya kanuni,” alisema.

Kwa upande wake Mohamed Ally alisema awali wafanyabiashara walikuwa na hofu, lakini sasa BoT imewaondolea.

“Awali mtu akiwa na fedha ya kigeni anakuwa na hofu kama ameshika bangi, lakini sasa tumeambiwa ni rahisi kufanya biashara,” alisema.

Akitoa mada katika mkutano huo, Meneja msaidizi katika kitengo cha fedha cha BoT, Omari Msuya aliwataka wafanyabiashara hao kufuata Sheria ya fedha za kigeni ya 1992 na kanuni zake ili kufanya biashara bila wasiwasi.

Alizitaja kanuni hizo kuwa pamoja na kifungu cha 5(a) na 6 ya sheria kinachoipa mamlaka BoT kusimamia na kuidhinisha biashara ya fedha za kigeni.

"Kifungu cha 7(a) cha sheria, Gavana anaweza kuweka kanuni na maelekezo na miongozo.
“Kwa sasa gavana ameshaweka kanuni, Kanuni za usimamizi wa maduka ya kubadilisha fedha, kwa mujibu wa kifungu cha 5(a) na 7.

Alitaja kifungu cha 4(1, 2) cha kanuni hizo akisema mtu yeyote haruhusiwi kufanya biashara ya fedha za kigeni bila kuwa na leseni, na atakayekwenda kinyume atakuwa ametenda kosa na ataadhibiwa kwa faini au kifungo kisichozidi miaka 14.


Akifunga mkutano huo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema watashirikiana na BoT na wafanyabiashara hao kuhakikisha sheria zinafuatwa.

Biteko aunda kamati kuchunguza

Wakati huohuo, kufuatia uhaba wa fedha za kigeni, jana Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko aliunda kamati ya watu tisa kuchunguza jambo hilo.

Dk Biteko aliyasema hayo jana, katika mkutano wake na wauzaji madini na kueleza masikitiko yake kuwa wamekosa mchango wa kusaidia upatikanaji wa fedha za kigeni, ikiwemo Dola licha ya kuwa na mauzo makubwa ya madini.

Waziri huyo alisema katika kipindi cha mwaka jana, Tanzania iliuza nje ya nchi madini kwa thamani ya Dola 952.9 milioni, lakini utafiti unaonyesha kiasi kilichoingizwa nchini ni kidogo ukilinganisha na mauzo, wakati sheria inataka wauzaji kuingiza fedha za kigeni na kuzibadilisha nchini.

Kiasi hicho kilisababisha Wizara kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa kutoka wastani wa asilimia 6.8 2021/22 hadi kufikia asilimia 9.1 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

“Hili haliwezekani, kuna wizi wa wazi, hatuwezi kuwa na hali hii, leo lazima tuunde kamati ya kufanya uchunguzi ili tujue fedha zilikokwenda ikiwa mauzo yanaonekana ni makubwa,” alisema Biteko.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments