“Tumeumbwa kusikilizwa; kusikika ni hitaji kubwa la mwanadamu. Tunatamani kueleweka hasa kwa watu wetu wa karibu.”
Hiyo ni kauli ya Mhadhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Christian Bwaya alipokuwa akizungumza kuhusu ukimya wa wenza ndani ya ndoa.
“Kwa wanandoa, kununiana huanza taratibu. Unamwambia jambo mwenzako unaona hana nia ya kuelewa upande wako, anakuwa mwepesi kukunyamazisha, kukukosoa au kugombana. Wakati mwingine mtu anarudia kilekile, huoni mabadiliko. Hii huweza kumfanya kusema haisaidii. Hali hii ikiendelea, kidogo kidogo mtu huanza kupoteza uhuru wa kuwasiliana na mwenzake. Huanza kuona bora anyamaze,” anasema Bwaya.
Anasema uhusiano wa watu wawili (wanandoa) unajengwa na uwezo wa kusema kwa uwazi kile wanachofikiri na ukisikiliza kinachosemwa na mwenzako bila kukihukumu unamfanya aendelee kuwa wazi zaidi kwako.
“Mwenzako akianza kujihisi hana sababu ya kusema, hali hii inaweza kusababisha upweke na unyonge unaoweza kuzalisha migogoro mingi kati ya wanandoa. Mtagombana kwa vitu ambavyo mngeongea ingekuwa rahisi kuelewana. Mtagombana kwa sababu zisizo za msingi kwa vile tu mnasumbuliwa na upweke na kujisikia ule unyonge wa ndani kwa ndani.”
Upendo, maelewano ndiyo nguzo
Bwaya anasema kikubwa kabisa ni kuelewa kuwa mwenzako anatamani kusikika, ukimpenda mtu utamsikiliza, “epuka kumkosoa mwenzako mara kwa mara. Mpe nafasi ya kusema na wakati mwingine tunza mtazamo wako tofauti kwanza mpaka utakapokuwa na hakika amejisikia kusikilizwa.”
Pia, anasema ni muhimu kujifunza kubadilika, mwenzako anaposema jambo, atafurahi kuona kile alichokisema umekifanyia kazi kwa kuwa, usipobadilika unatuma ujumbe kuwa alichokisema hakina maana.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema wanandoa kununiana ni jambo baya kwa sababu kwa kauli ya mtume Mohammad wanawake ni wenza wa wanaume.
“Kwa kauli hiyo, wanawake ni wenza wa wanaume, basi wanaume hao wanatakiwa kuishi nao kwa wema na kumbughudhi mtu sio wema,” anasema Sheikh Mataka.
Hata hivyo, anawataka wanaume wawaelewe wanawake, kulingana na Mungu alivyowaumba kwa kuwa kuna wakati wanatokea kuwaudhi waume zao bila kudhamiria.
“Kwa mwanamke kuna mambo mengi, ikiwamo kupata ujauzito, hali inayosababisha kuwa na mabadiliko hadi ya kitabia, hivyo unaweza kadhani kakusudia kumbe ni ile hali inayomfanya kukufanyia aliyokufanyia, hivyo usipokuwa makini kudadavua mambo haya, utajikuta unamnunia mwenza wako bila sababu, na je, akienda hali hiyo miezi tisa, ina maana utanuna mpaka ajifungue,” alihoji Sheikh Mataka.
Wadau wa ndoa wanasemaje?
“Unajua wanawake wanaongea sana, jambo kidogo analifanya linakuwa kubwa, ndio maana wakati mwingine huwa simjibu mke wangu halafu anadhani nimemnunia,” anasema mkazi wa Ilala aliyejitambulisha kwa jina moja la Hafidhi.
Hata hivyo, Helen Philip anasema yeye anapenda kusikilizwa pindi anapokuwa na jambo lake, lakini inapotokea hapewi muda anahisi ni dharau anafanyiwa tena na mtu wake wa karibu.
“Kitu ambacho sipendi ni mume wangu kunipuuza napomweleza jambo, tena la maana, hali hii hunifanya nisimuongeleshe hadi hasira zangu ziishe.”
Dharau yatajwa
Mwanasaikolojia Charles Mhando anasema mpaka inafikia sababu ya watu kununiana ndani ya ndoani kushuka kwa heshima baina ya wanandoa au wenza na kudharauliana, hasa pale mmojawapo anapojiona yupo juu zaidi ya mwenzake.
“Licha ya kuwepo dhana kuwa mume ndio kichwa cha familia, wakati mwingine dhana hii inatafsiriwa vibaya na baadhi ya wanaume kwa kujiona kuwa yupo sahihi hata kama kosa kafanya yeye,” anasema Mhando.
“Lakini pia kwa wanawake kutokana na haya masuala ya kupambania haki za binadamu na usawa wa kijinsia, naye anaweza akajiona yupo kwenye haki, hivyo kila mmoja anaona akinuna hakuna kitu mwenzie anaweza kumfanya kwa kuwa ana haki ya kufanya hivyo na wala hatakiwi kuomba msamaha.”
Anasema kuna haja ya mmojawapo kujishusha, jambo ambalo hata aliyekosa atajiuliza kwa nini mwenzangu kawa kimya, hivyo hiyo inasaidia mtu kutorudia wakati mwingine.
Jingine, Mhando anasema ni kila mmoja kuheshimu maamuzi ya mwenzake kwa kukaa pamoja kuzungumza na kushirikishana kwa kila hatua unapotaka kufanya jambo fulani.
“Kikubwa hapa ni kufanya mambo kwa usahihi, kuheshimiana na kusikilizana, lakini kubwa kumsoma mwenzako kujua hapendi nini, anapenda jambo gani na anapokasirika ni njia gani mbadala unaweza kutumia katika kuyamaliza,” anasema mwanasaikolojia huyo.
Anasema wenza wanatakiwa kutovipa nafasi vitu vidogo kuvifanya vikubwa, kwa kuwa wakati mwingine ukifuatilia sababu ya wao kununiana utakuta ni mambo madogo sana.
Pia, anawashauri waliofikia hatua hii kuepuka kulazimisha furaha mbele za macho ya watu ili waonekane wapo sawa na kutolea mfano wengine wanapokuja wageni, wanaigiza kuwa wapo sawa na kuonyesha ushirikiakiano, baada ya kuondoka wanarudia katika hali zao za kununiana jambo linaloumiza zaidi.
Kwa nini wanandoa hununiana?
Mhando anasema wapo wenye tabia za kununa pindi wanapoudhiwa, hivyo ni vema kumsoma mwenzako nini ukifanya unamuudhi ili kuepuka kufanya yatakayowafikisha huko.
“Na hapa ni vema kusomana tabia kabla ya kuingia kwenye ndoa, kuwa mwenza wako akinuna unawezaje kumrudisha katika hali yake ya kawaida.”
Pia, anasema kununa wakati mwingine ni tabia ya kutoka katika familia, hivyo hawezi kuiacha ila unaweza kuwa na nafasi ya kumtuliza ukishamjua vizuri.
Kauli hiyo inashabihiana na kile anachokisema mwanasaikolojia mwingine, Chris Mauki kuwa wengine hununa kutokana na mazoea katika ndoa, kwa kuwa ndoa mpya huwezi kukuta haya mambo.
Mauki anasema jingine linalosababisha kununiana ni kukosekana uaminifu kwa wanandoa.
Hata hivyo, anasema watu wanapaswa kuelewa kuwa kununiana ni alama ya kuwaonyesha wanaopendana kwamba, kuna tatizo baina yao.
“Kununiana ni signal (alama) ya kuwaonyesha wanandoa kuna kitu cha kukifanyia kazi au kuna kitu wamekisahau, pia kunaweza kukupa taarifa yamkini kuna mtu ameongezeka kati yenu, hivyo kuwa kama taa nyekundu inayoashiria hatari ili muweze kushughulikia suala lake,” anasema Mauki.
Mchambuzi wa Masuala ya Jamii na Familia, Charles Misango, anasema kununiana ni jambo la kawaida katika jamii kwa kuwa kila binadamu ana madhaifu yake, ingawa kwa watu wenye afya ya akili kuna kununiana na kunyamaziana.
“Yaani kuna wakati mtu hajanuna ila ameamua kunyamaza ili kuepusha shari na kwa anayefika hatua ya kununa ni ishara ya kuonyesha kuwa amekasirika na hapo kuna vitu atakuwa alikuwa akikufanyia utaona hatavifanya, ikiwamo kutoshiriki tendo la ndoa,” anasema Misango.
Nini madhara yake
Mwanasaikolojia huyo anasema, “msiposhughulikia kununiana hata ule ukaribu wenu unapungua na hata ikatokea mmoja akasafiri ile hamu ya kutaka kumuona huwezi kuihisi tena.
“Kununiana kusipofanyiwa kazi penzi linaweza kufa na ndoa kuvunjika au suala la kukosa uaminifu linaweza kutokea,” anasema Mauki.
Kuhusu athari, mwanasaikolojia Mhando anasema kuna hasara kubwa kwa wenza kununiana, kuna mambo yanaweza kusimama katika familia, mfano mwanamume anapoacha hela ya matumizi halafu akirudi anaikuta vilevile lakini mahitaji mengine yote anakuta yamefanywa.
“Hapa kuna mawili, ama mwanamke ana biashara zake na ili kumuonyesha mwanamume hana shida na hela yake, anamega mtaji wake na kutumia hela kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, fedha ambayo angeweza kufanyia jambo jingine la maendeleo,” anasema Mhando.
“Lakini kwa mwanamume inaweza kuwa nafasi ya kutoacha hela na kukwepa wajibu wake kwenye familia, jambo ambalo mwingine anaweza akapatia sababu ya kumwachia mwenzake mzigo wa kulea familia mwenyewe, hivyo kununiana kwa kweli kuna hasara kubwa kuliko faida,” anasema Mhando.
Nini kifanyike?
Hata hivyo, Mauki anashauri kuwa wanachopaswa kufanya waliofikia hapo, ni vizuri kujiwekea utaratibu ikitokea mmenuniana basi msifanye hivyo siku nzima.
“Yaani mmenuniana halafu inatokea mnafanya hivyo siku nzima, mmelala, mmeamka mnuno unaendelea, hivyo kwa kuweka sera hiyo ya kumaliza mnuno kutakapokucha itawasaidia.
“Katika suala la kisaikolojia tunasema mkilala mkiwa na furaha, mkilala mkiwa mmeshazungumza ni afya kwako na afya ya akili kwako wewe na itakusaidia kuamka kesho ukiwa tayari na siku nzuri yenye mafanikio, lakini kama utalala na maumivu basi utaamka nayo,” anasema Mauki.
Mchambuzi Misango anasema madhara ya kununiana ni makubwa, hasa kama mna watoto; kwa umri wao hujua mapema sana kuwa hakuna amani kwa wazazi, hivyo kama ni mtoto anampenda mama yake utaona anaanza kumchukia baba, “na kama anampenda baba ataanza kumchukia mama, jambo ambalo ni hatari katika makuzi yao na ubongo kwa jumla.”
“Hili linachangia kuwajazia hofu watoto katika maisha yao, licha ya kutakiwa kuwajaza vitu vya kujenga afya ya ubongo na afya yao ya mwili,” anasema Misango.
“Ijulikane wazazi wanapozungumza na kucheka, humjengea mtoto afya na ukuaji sahihi na kutamani atakapokuwa mkubwa kuwa kama wazazi wake, lakini kubwa linamjengea usalama na kumpa nafasi nyingine ya kuwaza vitu vikubwa zaidi, hivyo ni vema kuepuka kununiana.”
0 Comments