DAR ES SALAAM: Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema anakoshwa na namna wachezaji wa kikosi hicho wanavyotekeleza majukumu yao uwanjani na ndio siri kubwa ya ubora wa timu hiyo.
Ameyasema hayo leo Septemba 19, 2023 wakati akizungumzia maandalizi ya kuelekea mchezo wa ligi kuu siku ya kesho dhidi ya Namungo.
Amesema kwa jinsi kikosi hicho kinavyocheza hiyo ndiyo falsafa yake na muda mwingi anafurahia kucheza soka la kushambulia na kumiliki mpira.
Ameongeza kuwa anajivunia ukubwa wa kikosi chake hivyo kuna uwezekano kukawa na mabadiliko makubwa kwenye mchezo dhidi ya Namungo.
“Nina idadi kubwa ya wachezaji, tena wenye ubora, ninapenda kuwapa nafasi waoneshe ushindani, tunahitaji kutoa nafasi kwa kila mchezaji ili kuwa na utimamu wa wachezaji wetu” amesema Gamondi
Kocha huyo Muargentina ataiongoza Yanga kwenye mchezo wake wa tatu wa ligi kuu bara ambapo katika michezo miwili ya ligi iliyopita ameibuka na ushindi wa mabao matano kwenye kila mchezo.
0 Comments