Bashungwa ambana mkandarasi, atoa siku 14

 

MBEYA: Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara (TANROADS), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira/Itungi Port (km 32) analeta vifaa na watalaam wote wanaohitajika eneo la mradi kwa mujibu wa mkataba.
Mradi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 38 ambapo unatekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya M/s AVM-Dillingham Construction International na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS).
Bashungwa ametoa agizo hilo Oktoba 2, 2023 wilayani Kyela mkoani Mbeya mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ipo nyuma ya muda wa mkataba kwa asilimia 25 na kubaini mradi huo una upungufu wa watalaam na vifaa muhimu vinavyohitajika eneo la mradi.
“Naiagiza TANROADS, CRB na ERB kunipa taarifa ndani ya siku hizo na kama mkandarasi akishindwa kutekeleza kama mkataba unavyosema na tutalazimika kuchukua hatua ngumu basi tuzichukue haraka iwezekanavyo”, amesema Bashungwa.
 
Bashungwa ameeleza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekwishatoa fedha kiasi cha Bilioni 3.7 kama sehemu ya malipo ya kwanza ya awali ya ujenzi huo na hadi sasa mkandarasi amekwishafanya maandalizi kwa asilimia 15 tu ukilinganisha na mahitaji ya mkataba.
“Kama unataka kujua rangi ya Rais chezea hii hela aliyoitoa Dk.Samia… Mkandarasi umepewa hela ndo unaenda kufanya manunuzi ya vifaa Uturuki wakati ulitakiwa uwe navyo tayari na kuvileta eneo la mradi kipindi cha maandalizi”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa anafahamu mkandarasi huyo amepewa tena ujenzi wa barabara ya Sengerema – Nyehunge (km 54.4) ambapo ametilia shaka kasi ya mkandarasi huyo ambayo anaenda nayo  kama ataweza kutekeleza mradi huo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments