DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeongeza bajeti kwenye sekta ya michezo ili kuipaisha zaidi sekta hiyo huku dhamira kuu ikiwa ni kupata mafanikio makubwa zaidi.
Majaliwa ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2023 katika hafla ya kukabidhi hundi ya Sh milioni 500 kwa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa stars ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya timu hiyo kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast ambapo kiongozi huyo amesema serikali itaendelea kuunga mkono wanamichezo nchini kote.
Amesema kwa sasa mwamko ni mkubwa katika sekta ya michezo na haishangazi kuona Tanzania ikiwa kivutio kikubwa ulimwenguni na ndio maana kwa mara ya kwanza taifa hilo linakwenda kuandika historia ya kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika 2027.
Aidha Waziri Mkuu amesema baada ya kukagua ukarabati unaoendelea katika dimba la Benjamini Mkapa ameridhishwa na marekebisho yanayoendelea na kuwataka wadau wa michezo nchini kuitunza miundombinu ya uwanja huo ili uendelee kuwa katika ubora wake.
Pia Majaliwa amesema timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zitaendelea kupewa hamasa ya goli la Mama ili kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya taifa.
0 Comments