ARUSHA;MASHINDANO ya riadha ya Lake Manyara Marathon yamepangwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, yakilenga kutangaza utalii na kuibua vipaji vya riadha nchini.
Wanariadha 3000 wanatarajiwa kushiriki mbio hizo zitakazofanyika kwa mara ya kwanza katika mji wa Mto wa Mbu, Wilaya Monduli Mkoa wa Arusha.
Mwanariadha wa kimataifa, Emmanuel Giniki, ameteuliwa kuwa Balozi wa mbio hizo, na ni miongoni mwa washiriki wa Lake Manyara Marathon.
Makundi mbalimbali ya wanariadha kwa wanawake na wanaume yatahusika katika mbio za Kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5.
Mkurugenzi wa kampuni ya Greenleaf Mohar, ambao ndio waandaaji, Morris Okinda amesema mbio hizo zitaenda kufanyika kwa mara kwanza zikilenga kuibua na kutangaza utalii wa hifadhi ya Ziwa Manyara.
“Lengo ni kupata wachezaji watakaowakilisha taifa kimataifa na tunatarajia kuwa na taasisi ya ‘Posso International Sports’ kutoka Marekani, ambao watafika nchini kuangalia vipaji na hii itafungua fursa ya vijana kuonekana na wanariadha wetu wataweza kuwakilisha nchi wakiwa na kiwango cha kimataifa,”ameongeza Okinda.
0 Comments