DAR ES SALAAM: WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeandaa mkakati wa kuhakikisha sekta hiyo inachangia kiwango kikubwa cha pato la Taifa tofauti na sasa ambapo sekta hiyo inachangia asilimia saba.
Akizungumza leo Oktoba 13, 2023 Naibu Waziri wa Wizara hiyo Alexander Mnyeti katika mafunzo ya utambuzi wa mazao ya uvuvi katika Bahari na Maziwa pamoja na ukusanyaji takwimu, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) yatasaidia kupata taarifa sahihi juu ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini, lengo ni kuiwezesha sekta hiyo kuchangia zaidi katika Pato la Taifa
Tafiri inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Chuo Kikuu cha Duke cha nchini Marekani.
Mnyeti, amesema, mafunzo hayo yatawezesha kujua namna ya kukusanya takwimu katika sekta ya uvuvi, kujua idadi ya viumbe hai vilivyopo kwenye bahari na maziwa yaliyopo nchini.
“Ili uviendeleze na ulete mchango kwenye pato la Taifa, lazima ujue idadi yake iliyopo humo na vinazaliana vipi katika hali ya Ikolojia na Bailojia yao. ” Amesema Mnyeti na kuongeza
” Kwa hiyo lengo la kuizindua ‘workshop’ hii tunaenda kufahamu sasa data kamili namna ya kuzitunza, kuziandaa na kuzitumia, ili ziweze kuleta mchango katika uchumi.
Amesema sekta ya uvuvi bado ina mchango mdogo katika pato la Taifa ni asilimia 7 na wakati mwingine inashuka chini ya asilimia hiyo.
“Kwa sababu data hazijaboreshwa ndio maana tupo hapa kwenye workshop kwa lengo sasa tutakapozijua na kujua taarifa ya kilichopo ndani ndio tutajua namna ya kuzitumia zilete mchango katika Pato la Taifa.
“Duke University wametufundisha namna ya kwenda kutumia data zetu na kuzigeuza kuzileta kwenye Pato la Taifa.” Amesisitiza Mnyeti.
Aidha, amesema kwa sasa wanahamasisha watu wafungue viwanda vya kuchakata samaki.
“Hatuwezi kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi bila kuchakatwa minofu, wavuvi wapo wa kutosha ila viwanda ni vichache sana, Rais Samia Suluhu Hassan amefungua bandari ya uvuvi, tafsiri yake tutakua tunasafirisha minofu ambayo ipo tayari kwa matumizi ya binadamu sio samaki, kusafirisha samaki ni hasara ni kama usafirishe ng’ombe kwenye meli.
“Haina faida kwa Taifa wala kwa mfugaji, tunachotaka sasa hivi ni kusafirisha nyama kama tunavyosafirisha samaki kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi.
“Tunahamasisha watu wafungue viwanda Kwa wingi kusaidia kuchakata kwenye mnyororo wa thamani.”Amesisitiza Mnyeti
Mnyeti amewataka wachache waliopata mafunzo wakawafundishe wenzao ili wazalishwe wataalamu wengi wenye ujuzi wa kuzitumia takwimu hizo.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Tafiri Dk Mary Kishe amesema wanaangalia ni kwa namna gani takwimu za Tanzania zinasaidia uendelevu wa rasilimali za uvuvi.
” Lakini pia tunawezaje kuwashirikisha watunga sera ambao wanasimamia rasilimali zetu za uvuvi, lakini pia tumeangalia hizi takwimu zinatupa uhalisia wa mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa?
“Tumegundua kuna gepu, tumeweza kuzijaza, tumefanikiwa kuwaonyesha wenzetu wa Duke university takwimu zetu na idadi ya watu tulionao Tanzania, wametuhakikushia watawezesha kufanya mchakato mpya, wa kuangalia mchango wa uvuvi katika pato la Taifa.” Amesema Mary
Amesema, hiyo itasaidia serikali kuweka taarifa zake sahihi kulingana na idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya Tanzania ina watu milioni 60.
“Zitatusaidia kujua ni watu wangapi wamekua wakinufaika kupitia rasilimali zilizopo majini. ” Amesema Dk Mary
Mafunzo hayo yanaendeshwa na na wanasayansi na watafiti kutoka nchi 50 kuhakikisha rasilimali ambazo hazijionyeshi kwa uwazi ziweze kuonekana hususani kwenye uvuvi mdogo ili kuongeza michango wa sekta ya uvuvi katika pato laTaifa
Kwa upande wa Ofisa Mipango na Tafiti kutoka FAO, Nicole Franz amesema uwepo wa taarifa sahihi ni muhimu katika kuendeleza sekta ya uvuvi pamoja na kulinda rasilimali za uvuvi nchini
Amesema uwepo wa taarifa sahihi utawezesha pia kubadili maisha ya watu wanaojishughulisha na uvuvi hususani wavuvi wadogo kwa kuangalia namna wanavyochangia katika sekta hiyo kwa kuwa ni sekta inayochangia ongezeko la chakula duniani.
0 Comments