MANYARA: Rais Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Serikali ni kutengeneza vijana wenye mchango katika kukuza uchumi wa taifa ili kupunguza changamoto ya ajira.
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi 64 katika Wilaya mbalimbali nchini ili kuwapa vijana nafasi ya kutumia rasilimali zilizopo kujikwamua kiuchumi.
“Endapo tutakuwa na vijana wazembe, wazururaji wasiowajibika utakuwa mzigo kwa taifa letu, tunataka tujenge taifa lenye vijana wachapakazi wawajibikaji na wazalendo ili waweze kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa baada ya ujenzi wa vyuo hivyo 64 vya VETA Serikali itatengeneza vyuo vingine 50 ili kufikia lengo la kuwapa vijana ujuzi wa kuwa wajasirimali na kuingia katika Kilimo, Uvuvi na Ufugaji.
Rais, Samia ameyasema hayo leo Oktoba 14 katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 zilizofanyikia katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo katika mji wa Babati mkoani Manyara.
0 Comments