WAZIRI MKUU AWATAKA MADEREVA WA SERIKALI WAZINGATIE SHERIA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro, Oktoba 24, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 ………………..

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka madereva wa Serikali kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote kwa sababu kuendesha gari ya Serikali haimaanishi wamepewa rungu la kuvunja sheria bali wanapaswa kuwa mfano wa kuzizingatia hasa zile za usalama barabarani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, “ukiwa dereva wa Serikali haimaanishi kuwa uko juu ya sheria bali kila dereva anatakiwa kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote. Aidha,  madereva wa vyombo visivyo vya Serikali wanapaswa kujifunza kutoka kwenu madereva wa Serikali.”

Pia, Waziri Mkuu amesema madereva hao wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ya madereva wa Serikali ambayo yanawataka madereva hao kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani. “Madereva wa Serikali hakikisheni mnakuwa kioo cha jamii.”

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 24, 2023) alipofungua Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali, katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro. Kongamano hilo limebeba kauli mbiu isemayo; “Dereva wa Serikali bila ajali inawezekana. Kazi iendelee”

Akizungumzia kauli mbiu hiyo, Waziri Mkuu amesema ni kweli inawezekana kuendesha magari ya Serikali bila kusababisha ajali iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria zilizopo, hivyo amewasisitiza madereva hao wahakikishe wanafuata sheria.

“Ninawapongeza sana kwa kuwa kaulimbiu hii pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 105 (K) ambayo inailekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine kuendelea na jukumu la kudhibiti ajali za barabarani.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeshafanya jitihada kubwa katika kutatua kero za watumishi wa kada hiyo ya udereva na bado inaendelea kuzitatua changamoto zinazojitokeza kwa kushirikiana na Chama chao.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara zenye dhamana husika bila kuathiri shughuli na majukumu yake ya kila siku ya kiutumishi, imebadilisha muundo wa ajira na kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade test) katika kuwapandisha madaraja na ngazi za mshahara kwa mwaka wa fedha uliopita.

Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya tisa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi zinaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda maslahi ya madereva wa Serikali pamoja na kuyafanyia kazi maombi na ushauri utakaotolewa.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahakikishia madereva hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kupitia Chama Cha Madereva wa Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuongeza tija katika utendaji kazi Serikalini.

Pia, Waziri Bashungwa amesema suala la stahiki za madereva linapewa msisitizo mkubwa na Serikali. Kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, waajiri wote wahahakikishe kuwa madereva wote wanapatiwa barua za kuthibitishwa hususan kwa wale ambao bado hawajapewa barua hizo.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema wizara kwa kushirikiana na taasisi zingine za utumishi wa umma imejipanga kuhakikisha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kinaendelea kutoa mafunzo bora kwa madereva na maafisa usafirishaji pamoja na kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Serikali, Castro Nyambange pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade test) ambacho kilikuwa kikiwasababishia wasipande madaraja wala mishahara.

Kadhalika, Kaimu Katibu Mkuu hiyo ameiomba Serikali kuboresha malipo ya kufanya kazi masaa ya ziada yafanyike kwa wakati na bila upendeleo hususan madereva wa magari ya wagonjwa (Ambulance) na wanaowahudumia madaktari na manesi wanaokuwa zamu usiku.

Lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha madereva wa Serikali kutoka katika mikoa, halmashauri, taasisi za umma na mashirika ya umma nchini kujifunza masuala ya maadili ya udereva, kanuni na miongozo ya Serikali kwa ajili ya kukuza tasnia hiyo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji.

  

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro, Oktoba 24, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments