Mradi wa maji Uhambingeto wakamilika

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Iringa imefanikiwa kuukamilisha mradi wa maji wa Uhambingeto wilayani Kilolo mkoani Iringa, ulioshindwa kutekelezeka kupitia kampuni ya Mshamindi Construction Limited.

Wakazi zaidi ya 8,989 wa kijiji na kata ya Uhambingeto wameanza kufurahia huduma ya maji safi na salama waliyokuwa wameikosa kwa miaka yote tangu kijiji na kata hiyo ianzishwe.

Hatua hiyo imewezekana baada ya RUWASA Mkoa wa Iringa kulazimika kuumalizia mradi huo ulioonekana kushindwa kutekelezwa na mkandarasi huyo kwa wakati; kwa kutumia mafundi wa ndani.

Taarifa iliyotolewa na Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Kilolo, Mhandisi Enock Basyagile imesema kukamilika kwa mradi huo ni moja ya mafanikio ya ‘kujipiga kifua’ kwani kumeleta imani kubwa kwa wananchi.

“Wananchi wameamini kwamba serikali kwa kupitia RUWASA ina dhamira ya dhati ya kupunguza au kumaliza kabisa adha ya upatikanaji wa maji hususani kwa kina mama ambao takwimu zinaonesha ndio wamekuwa wakibebeshwa jukumu la kutafuta maji kwa matumizi makubwa ya majumbani,” alisema.

Mhandisi Basyagile alisema mradi huo umesanifiwa kuzalisha kiasi cha lita 5.81 za maji kwa sekunde jambo linatoa uhakika wa upatikanaji wa maji katika kata hiyo.

Aliwaomba wananchi wa kata hiyo kwa ujumla wake kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya mradi huo ili iwe na manufaa ya muda mrefu kwa wanufaika wote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA, Mhandisi Ruth Koya ameipongeza RUWASA Mkoa wa Iringa kwa kusimamia kwa uadilifu mradi huo akisema utakuwa na matokeo chanya kwa maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.

“Serikali imefanya jitihada kubwa sana hadi kuleta mradi hapa, na imewekeza fedha nyingi kuhakikisha huduma hii inawafikia.  Niwaombe wananchi msogeze maji majumbani mwenu na chama cha watumia maji msituangushe muhakikishe huduma hii inakuwa endelevu,” alisema Mhandisi Koya.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji na kata ya Uhambingeto wameishukuru serikali kwa kufikisha huduma hiyo karibu na makazi yao wakisema kilichobaki mbele yao ni kuisogeza majumbani mwao.

“Tulikuwa tunafuata maji kwenye mito midogo ambayo wakati wa kihangazi kikali ukauka kabisa na hivyo kutulazimu kutafuta huduma hivyo vijiji vya mbali na kununua kwa kati ya Sh 2000 na Sh 5000 kwa ndoo ya lita 20 jambo lililokuwa linatuongezea gharama za maisha,” alisema Francisca Chengula mkazi wa  Uhambingeto

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jema Lyego alisema huduma bora ya maji itawasaidia kupunguza hatari za magonjwa yanayosababishwa na maji machafu, wataokoa muda wa kutafuta maji kwa kufanyashughuli zingine za maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii kukua na kuendeleza miundombinu mingine kama shule na hospitali.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments