KAGERA: WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameungana na wananchi wa Wilaya ya Karagwe na Mkoa Kagera katika hafla ya kumpongeza na kumkaribisha nyumbani Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, baada ya kuteuliwa na kusimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali.
Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Kasheshe, Nyaishozi wilayani Karagwe mkoani Kagera na kuhudhuria na viongozi mbalimbali wa Dini na Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, ambapo pamoja na mambo mengine Waziri Bashungwa ametoa salamu za pongezi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa Kardinali Rugambwa.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anaungana na Watanzania kuendelea kumpongeza Kardinali kwa heshima hii ambayo nchi yetu tumeipata, amenipa dhamana ya Wizara ya Ujenzi na baada ya kuona mawasiliano barabara ya kuja hapa Kasheshe yalivyokuwa,..
Sisi tulijiongeza ili tusimuangushe Rais tukatengeneza barabara ili wageni watakaotoka sehemu mbalimbali wafike hapa kwa urahisi kwa kumpongeza Kardinali” amesema Bashungwa.
Aidha,Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kumuombea Kardinali Rugambwa heri, afya njema, na mafanikio katika utumishi wake.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema Mkoa wa Kagera una bahati sana kwani umeweza kumtoa Kardinali na hiyo ni heshima ya kipekee ambayo itasaidia Mkoa wa Kagera kuwa na wacha Mungu na kuepuka yote yaliyokatazwa kwenye maandiko matakatifu.
Naye, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa amewashukuru wananchi wa Kagera kwa kumpokea na kuwasihi Watanzania kuendelea kumtegemea Mungu kwa kila jambo ili waweze kuvuna mema.
0 Comments