CCM yaelekeza ulinzi kwa wabunge

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetoa tamko kwa viongozi wa chama hicho kwenye mikoa na serikali kuwalinda wabunge wa CCM waliopo madarakani ili waweze kutekeleza majukumu yao badala ya kusumbuliwa na wanachama wanaotaka kugombea kwenye majimbo hayo kwenye uchaguzi ujao kwani muda wa kufanya hivyo haujafika.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu ametoa kauli hiyo  kwenye mkutano mkuu wa jimbo la Muhambwe Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma akimwakilisha  Kaimu Katibu Mkuu wa CCM, Anamringi Macha.

Gavu alisema kuwa wabunge wanaofanya kazi nzuri kama alivyofanya Dk.Samizi wanapaswa kulindwa na kupewa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo kutekeleza ilani ya uchaguzi waliyonadi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu (kushoto) akikabidhi hati ya utendaji bora kwa mbunge wa jimbo la Muhambwe Wilaya ya Kibondo Dk. Florence Samizi (kulia) baada ya mbunge huyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitatu

Katibu huyo wa Organaizeshani alisema kuwa wabunge na viongozi waliopo madarakani wako hapo kwa baraka za CCM hivyo chama hakitakubali kuona viongozi wenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi na kusimamia maelekezo ya serikali wakisumbuliwa na watu wenye nia na uroho wa madaraka.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi alizofanya Mbunge  wa jimbo la Muhambwe wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Dk.Florence Samizi amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu akiwa mbunge anajivunia kazi kubwa aliyofanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi kwenye jimbo hilo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM.

Dk.Florence Samizi Mbunge wa jimbo la Muhambwe Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya jimbo hilo kwa miaka mitatu akiwa mbunge wa jimbo hilo
Dk.Samizi akizungumza katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na  Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa amefanya kazi kubwa kwa kuchochea maendeleo ya jimbo kwa kutoa fedha kutoka vyanzo mbalimbali  ikwemo kiasi cha Sh milioni 152 kutoka mfuko wa jimbo ambapo pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo yeye binafsi pia ameshiriki kwenye shughuli mbalimbali za jimbo hilo.

Mbunge huyo  alisema kuwa kazi aliyofanya kwa kipindi hicho imewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, ujenzi wa madarasa,vyoo,mabweni,ofisi za walimu na nyumba za walimu huku miradi ya maji ikiwa sehemu ya kipaumbele ya utekelezaji wa miradi yake.

Sambamba na hilo alisema kuwa kazi kubwa pia imefanyika kwenye sekta ya afya kwa kuimarisha miundo mbinu ya huduma kwenye vituo vya huduma vilivyokuwepo, ujenzi wa zahanati mpya vijijini na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miundo mbinu ya barabara vijijini na suala la kupeleka umeme kwa wananchi vijijini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments